Watu 8 wauawa wakiwemo raia sita wa Ufaransa katika hujuma Niger
(last modified Mon, 10 Aug 2020 07:54:51 GMT )
Aug 10, 2020 07:54 UTC
  • Watu 8 wauawa wakiwemo raia sita wa Ufaransa katika hujuma Niger

Watu wanane, wakiwemo raia sita wa Ufaransa, wameuawa nchini Niger katika hujuma iliyotekelezwa na watu wenye silaha, Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa, waandesha pikipiki waliokuwa na bunduki waliwashambulia Wafaransa pamoja na raia wengine wawili wa Nigeria waliokuwa nao katika katika hifadhi ya Twiga karibu na mji wa Koure ulio kilomita 65 kutoka mji mkuu, Niamey. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo.

Gavana wa eneo la Tillaberi amesema genge hilo lilitekeleza hujuma ya kuvizia na kuwaua wote walikuwa katika msafara huo.

Ufaransa imethibitisha kwamba Wafaransa wameuawa katika shambulio hilo lililotokea jana Jumapili. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia amezungumza kwa simu na mwenzake wa Niger, Mahamadou Issoufou kuhusu tukio hilo.

Wizara ya mambo ya ndani ya Niger imesema kuwa operesheni ya kusaka majambazi hao inaendelea, ambapo jeshi la Barkhane linashiriki.

Rais wa Niger Mahamadou Issoufou, ambaye alizungumzia "shambulio la kigaidi na kikatili", ameongea kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kutoa salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga.

Wapiganaji ambao wanafungamana na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na ISIS au Daesh wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi katika miaka ya hivi karibuni pamoja na kuwepo maelfu ya wanajeshi wa kieneo na kimataifa wanaolinda doria katika eneo hilo. Ufaransa imetuma maelfu ya askari katika eneo la Sahel kwa kisingizio cha kupambana na magaidi lakini ugaidi unazidi kuongezeka eneo hilo.

Tags