Amnesty International yataka kufanyike uchunguzi kuhusu kifo cha al Aryan
(last modified Fri, 14 Aug 2020 13:04:10 GMT )
Aug 14, 2020 13:04 UTC
  • Issam al Aryan
    Issam al Aryan

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Misri ifanye uchunguzi kuhusu mazingira ya kutatanisha yanayohusiana na kifo cha mmoja wa viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin akishikiliwa katika jela ya Tora mjini Cairo.

Taarifa iliyotolewa na Amnesty International imesema maafisa wa serikali ya Misri wanapaswa kutoa amri ya kufanyika uchunguzi haraka kuhusu kifo cha Issam al Aryan, aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa harakati ya Ikhwanun Muslimin, katika jela ya Cairo. 

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu pia limewataka viongozi wa Misri kuwaachia huru wanaharakati na watetezi wote wa haki za binadamu wanaoendelea kushikiliwa katika jela na magereza za nchi hiyo.

Taarifa ya Amnesty international imesema kuwa: Kabla ya kufariki dunia, Issam al Aryan alikuwa amesema katika vikao vya kesi yake mahakamani kwamba ananyimwa huduma za tiba ndani ya jela, na kwamba anasumbuliwa na mienendo mibaya katika seli ya mtu mmoja na kunyimwa chakula cha kutosha na vifaa vya afya vya mtu binafsi. 

Taasisi hiyo ya kimataifa imesema kuwa kifo cha kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Ikhwanul Muslimin ni kengele ya tahadhari kuhusu hali ngumu ya wafungwa katika jela za Misri hususan kuhusu huduma mbaya za afya na hatari ya maambukizi ya virusi vya corona. 

Vyombo vya habari vya Misri vilitangaza kuwa, Issam al Aryan aliaga dunia jana Alkhamisi katika jela ya kutisha ya Tora ya Cairo kutokana na matatizo ya moyo. 

Issam al Aryan akiwa jela, Misri

Al Aryan alitiwa nguvuni mwaka 2013 baada ya mapinduzi ya jeshi yaliyoongozwa na jenerali Abel Fattah al Sisi dhidi ya serikali ya kwanza kuchaguluwa kidemokrasia nchini Misri ya Muhammad Morsi.

Al Aryan ni miongoni mwa viongozi wa Ikhwanul Muslimin waliokuwa wamekuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma kadhaa zinazohusiana na masuala ya kiusalama.

Al Aryan anajiunga na viongozi na mamia ya wanaharakati wa upinzani nchini Misri walioaga dunia wakiwa jela kutokana na kunyimwa huduma za matibabu na kutelekezwa.  

Rais wa zamani wa nchi hiyo Mohammad Morsi pia alianguka chini na kufariki dunia akiwa kwenye chumba cha mahakama tarehe 17 Juni mwaka jana nchini Misri.  

Wakati huo mashirika ya kutetea haki za binadamu yalisema: Mauaji yanayofanyika kwa kunyimwa huduma za tiba ndani ya jela na mahabusu za Misri yangali yanaendelea na yanachukua roho za wafungwa wa kisiasa kwa mpangilo na mfumo maalumu. 

Tags