Wapinzani Ivory Coast waendelea kupinga “muhula wa tatu” urais cha Ouattara
Makundi na vyama vya upinzani nchini Ivory Coast vimeendelea kupinga vikali uamuzi wa rais wa nchi hiyo, Alassane Ouattara wa kugombea tena kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo.
Mrengo wa upinzani nchini Ivory Coast unasema uamuzi wa Rais Alassane Ouattara wa kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu unakiuka katiba na utasababisha machafuko katika nchi hiyo ambayo bado inajikwamua kutoka kwenye vita vya ndani.
Ijumaa ya jana waandamanaji waliteketeza moto basi na magari kadhaa mjini Abidjan baada ya maandamano makubwa yaliyofanyika mapema wiki hii ili kupinga uamuzi wa rais wa kugombea muhula wa tatu. Waandamanaji hao wameapa kuchukua hatua zaidi dhidi ya uamizi huo wa Rais Ouattara.
Takwimu rasmi zilionyesha, watu watano wameuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika maandamano ya siku za hivi karibuni.
Katika machafuko ya Ijumaa ya jana, mabaki ya matairi yaliyochomwa moto yalitanda kwenye ngome ya upinzani ya Bonoua, wakati wakazi wa eneo hilo walipofanya maandamano mbele ya kituo cha polisi cha mji huo ambacho kilichomwa moto na waandamanaji siku kadhaa zilizopita baada ya mmoja wao kupigwa risasi.
Rais Alassane Ouattara amesema kuwa atagombea tena katika uchaguzi wa Oktoba 31 hatua ambayo imekosolewa kuwa anafuata nyayo za baadhi ya viongozi wa Kiafrika ambao walikanyaga katiba za nchi zao ili kusalia madarakani.
Katiba ya Ivory Coast inarusu kiongozi kuwa rais wa nchi kwa mihula miwili tu. Hata hivyo Ouattara amesema kuwa katiba mpya iliyoidhinishwa mwaka 2016 inatoa mwanya wa yeye kugombea tena kiti cha urais kwa mara ya tatu.