Harakati ya Kenya-Palestina yalaani mapatano ya UAE na Israel
Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imelaani vikali mapatano yaliyofikiwa baina ya watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel chini ya usimamizi wa makundi ya Kizayuni nchini Marekani.
Katika taarifa, Kenne Mwikya, Katibu wa Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina amesema, baada ya miaka mingi ya uhusiano wa siri baina ya tawala za Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu, pande mbili hatimaye zimefikia mapatano ambayo yatapelekea kuanzishwa uhusiano chini ya usimamizi wa serikali ya Trump.
Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imesema mapatano hayo yatatumika kuimarisha utawala wa Kizayuni ambao unakalia ardhi za Palestina kwa mabavu sambamba na kuwapa nguvu watawala wa Kiarabu ambao wanafanya jinai dhidi ya watu wa Yemen, Libya, Syria na Iraq.
Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji uhusiano wa kawaida kati ya UAE na utawala haramu wa Kizayuni, Alkhamisi iliyopita pande hizo mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.
Taarifa ya Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imesema mapatano hayo hayana maslahi kwa watu wa eneo la magharibi mwa Asia bali ni kwa maslahi ya tawala hizo mbili.
Kenne Mwikya ameongeza kuwa Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina inajiunga na Wapalestina kuwalaani viongozi wa UAE ambao wamewasaliti Wapalestina katika mapambano yao ya uhuru.
Hali kadhalika Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imetoa wito wa kususiwa Umoja wa Falme za Kiarabu hasa matamasha ya kiutamaduni, kiuchumi na kimichezo ambayo hufanyika katika nchi hiyo ya Kiarabu. Taarifa hiyo aidha imesisitiza udharura wa kususiwa safari zote kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).