Mazungumzo ya viongozi wa Sudan na Misri kuhusu Bwawa la An-Nahdhah
Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouli amefanya mazungumzo na mwenzake wa Sudan Abdalla Hamdok kuhusiana na Bwawa la An-Nahdhah au Grand Renaissance Dam (GERD) lililojengwa na Ethiopia.
Viongozi hao wametoa taarifa ya pamoja baada ya mkutano wao mjini Khartoum Jumamosi na kusema wana matumaini kuwa mazungumzo ya nchi hizo mbili na Ethiopia kuhusu ujenzi wa Bwawa la An-Nahdhah yatazaa matunda. Bwawa hilo kubwa zaidi barani Afrika ambalo linajengwa katika Mto wa Nile karibu kilomita 15 kutoka katika mpaka wa Ethiopia na Sudan limeibua mgogoro mkubwa baina ya nchi hizo tatu.
Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo limegharimu karibu dola bilioni nne utapunguza maji yanayofika katika nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu. Ethiopia nayo inasisitiza ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza katika nchi za nje.
Mazungumzo baina ya nchi hizo tatu yalikwama wiki iliyopita baada ya serikali ya Ethiopia kusisitiza kuhusu kujadiliwa upya mapatano ya kugawanya maji ya Mto Blue Nile.
Baada ya mazungumzo na mwenzake wa Misri, Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok amesema njia pekee ya kutatua mgogoro wa bwawa hilo ni mazungumzo.
Afrika Kusini, ambayo inashikilia uwenyekiti wa Umoja wa Afrika, imetoa wito kwa nchi hizo tatu kuendeleza mazungumzo kuhusu bwawa hilo.
Asilimia 90 ya watu milioni 100 wa Misri wanategemea maji wa Mto Nile na kwa msingi huo ujenzi wa bwawa katika mto huo unatazamwa na Misri kama tishio kwa uhai wake.
Mwezi uliopita Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema nchi yake tayari imeshafikia lengo la mwaka wa kwanza la kujaza maji katika bwawa hilo kufuatia msimu wa mvua kubwa.