Amnesty: Misri inawanyima wafungwa haki zao kwa miaka kadhaa sasa
(last modified Fri, 21 Aug 2020 00:07:39 GMT )
Aug 21, 2020 00:07 UTC
  • Amnesty: Misri inawanyima wafungwa haki zao kwa miaka kadhaa sasa

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Misri kuziruhusu familia za wafungwa kutembea jamaa zao wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo wakiwemo watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati wa masuala ya kisiasa.

Amnesty International imesema kuwa, serikali ya Misri inawanyima makumi ya wafungwa wanaoshikiliwa jela kukutana na watu familia na mawakili wao kwa miaka mingi.
Taarifa ya Amnesty International imesema Idara ya Magereza ya Misri inawazuia wafungwa wa kisiasa kuasiliana hata kwa barua na watu wa familia zao tangu familia zao zilipozuiwa kukutana nao. 
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeituhumu serikali ya Misri kuwa inawawekea vizingiti, kuwatesa na kuwanyima wafungwa haki zao kutokana na itikadi zao za kisiasa. 
Vilevile limeitaka serikali ya Cairo kuwaachia huru mara moja na bila ya masharti wafungwa wote wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu wanaoshikiliwa jela kwa sababu ya kutekeleza haki zao za kisheria. 

Miezi kadhaa iliyopita shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty international lilitangaza kuwa, maafisa wa serikali ya Misri wanawatia nguvuni na kuwafunga jela maelfu ya raia kwa tuhuma zisizojulikana zinazohusiana na ugaidi.

Taarifa iliyotolewa na Amnesty International imesema kuwa, maafisa wa serikali ya Misri wanatumia vibaya sheria ya kupambana na ugaidi kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani maelfu ya raia wanaokosoa utendaji wa serikali ya Cairo.

Taarifa hiyo imelaani kamatakamata na ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya dola nchini Misri dhidi ya wakosoaji na kusema Misri imekuwa jela kubwa kwa wapinzani wa utawala wa Rais Abdel Fattah al Sisi.

Tags