Watoto 10 wafa kwa kupigwa na radi nchini Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63095-watoto_10_wafa_kwa_kupigwa_na_radi_nchini_uganda
Watoto kumi wameaga dunia baada ya kupigwa na radi wakati wakicheza mpira wa miguu katika mji wa Arua, kaskazini magharibi mwa Uganda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 29, 2020 02:24 UTC
  • Watoto 10 wafa kwa kupigwa na radi nchini Uganda

Watoto kumi wameaga dunia baada ya kupigwa na radi wakati wakicheza mpira wa miguu katika mji wa Arua, kaskazini magharibi mwa Uganda.

Inaarifiwa kuwa, watoto 9 wenye umri kati ya miaka 13 na 15 walifariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na umeme wa radi, huku mwingine mmoja akipoteza maisha akiwa njiani akipelekwa hospitalini.

Habari zaidi zinasema kuwa, watoto hao walilazimika kujikinga mvua katika kijumba kidogo, baada ya kushadidi radi na kimbunga wakati walipokuwa wakicheza soka.

Watoto watatu wamenusuriki katika janga hilo la kimaumbile na wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya kieneo.

Umeme wa radi

Eneo la kaskazini magharibi mwa Uganda kwa siku kadhaa sasa linashuhudia mvua kubwa, vimbunga na radi.

Itakumbukwa kuwa, mwaka 2011, watoto 18 waliuawa kwa kupigwa na radi wakiwa shuleni katika eneo la magharibi ya kati nchini Uganda. Mwaka huo huo, watu wengine 28 walipoteza maisha kwa kupigwa na radi katika maeneo tofauti ya Uganda ndani ya wiki moja.