Jeshi la Misri laangamiza magaidi zaidi ya 70 Sinai Kaskazini
(last modified Tue, 01 Sep 2020 02:32:24 GMT )
Sep 01, 2020 02:32 UTC
  • Jeshi la Misri laangamiza magaidi zaidi ya 70 Sinai Kaskazini

Jeshi la Misri limetangaza kuwa limeua magaidi zaidi ya 70 wenye mfungamano na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) katika operesheni za vikosi vya usalama vya nchi hiyo katika mkoa wa Sinai Kaskazini.

Taarifa ya jeshi hilo imesema magaidi 73 waliuawa katika operesheni kadhaa ya vikosi vya serikali dhidi ya ngome na maficho ya magaidi hao katika Peninsula ya Sinai, baina ya Julai 22 na Agosti 30 (jana Jumapili).

Taarifa hiyo bila kutoa maelezo ya kina imeongeza kuwa, magaidi wengine wanne wameuawa huku askari saba wa Misri pia ama wakiuwa au kujeruhiwa katika operesheni hizo.

Mapigano huwa yanatokea mara kwa mara baina ya magenge ya kigaidi na jeshi la Misri katika mkoa wa Sinai ulioko kaskazini mwa nchi hiyo na katika baadhi ya maeneo mengine ya Misri.

Wanachama wa ISIS katika mkoa wa Sinai ya Kaskazini nchini Misri

Hapo jana, wanajeshi wanane wa Misri waliuawa katika mlipuko wa bomu uliotokea katika njia ulipokuwa ukipita msafara wa wanajeshi hao katika mkoa wa Sinai ya Kaskazini nchini humo.

Aidha wanajeshi wengine watatu wa jeshi la Misri waliuawa na wanne walijeruhiwa hiyo jana katika mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na magaidi katika mkoa huo.

Tags