Human Rights Watch: Hali katika jela za Misri ni mbaya
Shirika la kimataifa la haki za Binadamu, Human Rights Watch limetangaza habari ya kupoteza maisha wafungwa wanne katika kipindi cha chini ya masaa 72 kwenye jela za Misri na kusema kuwa hali katika jela hizo ni mbaya hasa kutokana na kudharauliwa usalama wa kiafya wa wafungwa.
Gazeti la al Quds al Arabi limeripoti habari hiyo likimnukuu Joe Stork, Naibu wa Mkuu wa Kitengo cha Asia Magharibi na Afrika Kaskazini cha shirika la Human Rights Watch akisema kuwa, wafungwa katika jela za Misri wanaendelea kufa ovyo licha ya kuweko maombi yanayosisitiza kuboreshwa huduma zao za afya. Vifo vya kiholela vya wafungwa hao vinaoensha jinsi maafisa wa jela nchini Misri wasivyojali usalama wa kiafya wa wafungwa.
Shirika hilo la kimataifa la haki za binadamu pia limesema katika taarifa yake kwamba, wafungwa wanne walifariki dunia katika kipindi cha chini ya masaa 72 baina ya tarehe 31 Agosti hadi tarehe pili Septemba na kuongeza kuwa, Ahmad Abdul Nabi Mahmoud (62) alifariki dunia tarehe pili Septemba 2020 katika jela ya Tarah baada ya kuweko katika jela hiyo kwa takriban miaka miwili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, raia wengine watatu wa Misri wamefariki dunia wakiwa kwenye jela mbalimbali za nchi hiyo katika kipindi cha masaa hayo.
Kabla ya hapo pia wanaharakati wa kisiasa walikuwa wameanzisha kampeni mbalimbali katika mitandao ya kijamii za kuwatetea wafungwa wa Misri chini ya kaulimbiu: "Rasilimali ya Seli za Jela."
Moja ya malengo ya kampeni hizo ni kushinikiza kuboreshwa hali za jela na kuhakikisha kunatolewa ruhusa ya kupelekewa wafungwa nguo nzito wa kuwakinga na barini wakati wa baridi kali.