Mawakili: Mtoto wa Morsi aliuawa kwa kemikali ya sumu Misri
Mawakili wa familia ya Mohammad Morsi, rais wa zamani wa Misri wamesema mtoto wa kiume wa kiongozi huyo, Abdullah Morsi aliuawa kwa kemikali hatari ya sumu, na wala hakufa kwa mshtuko wa moyo kama zilivyotangaza mamlaka za nchi hiyo ya Kiarabu.
Mawakili wa familia ya Mohammad Morsi wamesema kuwa hawana imani na uchunguzi uliofanywa na serikali na kusisitiza kuwa, mtoto huyo wa mwisho wa Morsi aliuawa kwa kudungwa kemikali ya sumu.
Abdullahi Morsi aliaga dunia Septemba 4 mwaka jana katika hospitali moja mjini Giza, kusini magharibi mwa mji mkuu Cairo, kwa kile kilichosemwa kuwa ni matatizo ya moyo.
Taarifa ya mawakili hao imesema: "Abdullah alizungushwa akiwa kwenye gari lake zaidi ya kilomita 20 na kupelekwa katika hospitali alikofia baada ya kuchomwa sindano yenye sumu angamizi. Kwa makusudi hawakumpeleka katika hospitali ya karibu."
Kundi la Ikhwanul Muslimin la Misri limekuwa likisisitiza kuwa, Abdullah Morsi, 26, alikuwa bado ni kijana mbichi, hivyo kudai kuwa kifo chake kimesababishwa na mshituko wa moyo ni jambo linalotia wasiwasi sana.
Oktoba mwaka juzi, vyombo vya usalama vya Misri vilimtia nguvuni Abdullah Morsi na kumwachia huru baadaye. Mtoto huyo wa kiume wa rais wa zamani wa Misri pia mwaka 2015 alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na aliachiwa huru baada ya kutumikia kifungo hicho.
Baada ya Muhammad Morsi kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa vyombo vya dola mwezi Juni mwaka jana, Abdullah Morsi aliituhumu serikali ya Cairo kuwa imemuua baba yake.