Wauguzi Zimbabwe wamaliza mgomo wao wa miezi mitatu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63320-wauguzi_zimbabwe_wamaliza_mgomo_wao_wa_miezi_mitatu
Chama kikuu cha wauguzi nchini Zimbabwe kimetangaza leo Jumatano kwamba kinawahamasisha wanachama wake kumaliza mgomo wao wa kulalamikia mishahara yao ambao ulianza mwezi Juni mwaka huu. Mgomo huo wa miezi mitatu umezilazimisha hospitali kuu za nchi hiyo kushindwa kupokea wagonjwa tena wakati huu wa janga la COVID-19.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 09, 2020 11:45 UTC
  • Wauguzi Zimbabwe wamaliza mgomo wao wa miezi mitatu

Chama kikuu cha wauguzi nchini Zimbabwe kimetangaza leo Jumatano kwamba kinawahamasisha wanachama wake kumaliza mgomo wao wa kulalamikia mishahara yao ambao ulianza mwezi Juni mwaka huu. Mgomo huo wa miezi mitatu umezilazimisha hospitali kuu za nchi hiyo kushindwa kupokea wagonjwa tena wakati huu wa janga la COVID-19.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, mfumuko wa bei nchini Zimbabwe ni zaidi ya asilimia 800, hali ambayo inakumbushia mazingira magumu ya zaidi ya muongo mmoja nyuma wakati mfumuko mkubwa mno wa bei uliposafisha akiba na marupurupu yote nchini humo.

Chama cha Wauguzi Zimbabwe (ZINA) ambacho kina zaidi ya wanachama 16,000 kiliitisha mgomo ili kumlazimisha Emmerson Mnangagwa kuwalipa wauguzi kwa sarafu ya dola ya Marekani lakini viongozi wa Zimbawe wanasema hawana uwezo huo.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

 

Mgomo huo wa wauguzi na madaktari wakubwa umekwamisha shughuli za hospitali za umma huku wagonjwa wote wasio mahututi wakiwa hawapokewi kwenye hospitali hizo huku idadi ya akina mama walioharibu ujauzito wao ikiongezeka kutokana na kukosa huduma zinazotakiwa za kiafya.

Mkuu wa chama hicho cha wauguzi, Enoch Dongo amesema kuwa, wameamua kusitisha kwa muda mgomo huo ili kumpa nafasi Makamu wa Rais, Constantino Chiwenga kutatua mgogoro huo. Ikumbukwe kuwa mwezi uliopita wa Agosti, Chiwenga aliteuliwa kuwa waziri wa afya wa Zimbabwe.

Amesema, kila mwezi wauguzi wanalipwa dola 6,000 za Zimbabwe, sawa na dola 73 za Kimarekani ikiwa ni pamoja na marupurupu. Hata hivyo takwimu za matumizi katika maisha ya kawaida ya Zimbabwe zinaonesha kuwa, familia ya watu watano inahitaji kwa uchache dola 15,573 za Zimbabwe ili isihesabiwe kuwa ni familia maskini. 

Waziri Chiwenga amesema, karibuni hivi serikali ya Zimbabwe itaacha kuwalipia mawaziri matibabu ya nje ya nchi na itatoa jedwali maalumu ya mapendekezo yake kwa sekta ya afya.