OCHA: Mafuriko ya Sudan yameua watu 103, nusu milioni wameathiriwa
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa zaidi ya watu nusu milioni wa Sudan wameathiriwa na mafuriko makubwa yanayoikumba nchi hiyo kutokana na mvua kali zilizosababisha kujaa maji ya Mto Nile.
Taarifa iliyotolewa na OCHA imesema kuwa, hadi Jumanne iliyopita zaidi ya watu laki tano na 57 elfu walikuwa wamedhuriwa na mafuriko nchini Sudan na kwamba maeneo ya Khartoum, kaskazini mwa Darfur na Sinar ndiyo yaliyopata hasara kubwa zaidi kutokana na mafuriko hayo.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa zaidi ya nyumba laki moja na elfu 11 zimesombwa na mafuriko ya sasa nchini Sudan.
OCHA imetangazarisha kuwa mvua kali zinazoendelea kunyesha nchini Sudan zinatishia kuzusha maradhi ya kuambukiza na kukwamisha juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
OCHA imesema hadi sasa watu wasiopungua 103 wameaga dunia katika mafuriko ya Sudan na wengine 56 wamejeruhiwa.
Tarehe 5 mwezi huu wa Septemba Baraza la Usalama wa Taifa la Sudan lilitangaza hali ya hatari kote nchini humo kutokana na mafuriko makubwa yanayoikumba nchi hiyo. Sudan pia imeomba msaada wa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathiriwa na mafuriko nchini humo.