Mchakato wa kuwapokonya silaha waasi wa FRPI huko DRC wakwama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63386-mchakato_wa_kuwapokonya_silaha_waasi_wa_frpi_huko_drc_wakwama
Wakazi wa mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameendelea kuwa na wasiwasi na hali inayojiri katika mkoa huo, baada ya kukwama kwa mchakato wa kuwarejesha waasi wa FRPI katika maisha ya kiraia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2020 21:53 UTC
  • Mchakato wa kuwapokonya silaha waasi wa FRPI huko DRC wakwama

Wakazi wa mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameendelea kuwa na wasiwasi na hali inayojiri katika mkoa huo, baada ya kukwama kwa mchakato wa kuwarejesha waasi wa FRPI katika maisha ya kiraia.

Mwishoni mwa mwezi wa Februari mwaka huum kundi la waasi la FRPI lilitia saini mkataba wa amani ulioelezwa kama "wa kihistoria" na serikali ya Congo. Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa  katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO na wadau mbalimbali walikuwa mashahidi, na walikaribisha kupigwa hatua katika mchakato wa amani katika mkoa huo wa Ituri.

Tangu wakati huo, mchakato huo umekwama na wakazi wanahofu kwamba wanamgambo hao huenda wakarejea msituni.

Zoezi la kuwapokonya silaha waasi hao lilitarajiwa kuanza mapema mwezi Mei, hata hivyo tangu wakati huo, hakuna kilichofanyika. Wanamgambo wenye silaha bado wako Azita, karibu kilomita 10 kutoka mji wa Gety, katika eneo la Irumu.

Wapiganaji wa ADF moja ya makundi ya waasi linaloendesha harakati zake kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Kwa upande wake, Kikosi cha Kusimamia Aani cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, kimesema kuwa,kimeweka maeneo ya ambayo watapokelewa wanamgambo hao, lakini ujumbe huo kwanza unataka waasi hao kupokonywa silaha ili kuweza pia kuweka mchakato wa kuwaingiza katika idara za usalama na ulinzi. Vyanzo vya serikali vinashutumu kundi la FRPI kwa kuuja na madai mapya ambayo hayakuwa kwenye mkataba.

Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.