Mafuriko yaua watu zaidi ya 70 nchini Nigeria
(last modified Fri, 18 Sep 2020 08:06:47 GMT )
Sep 18, 2020 08:06 UTC
  • Mafuriko yaua watu zaidi ya 70 nchini Nigeria

Kwa akali watu 77 wameaga dunia kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Nigeria.

Duru za habari zinaarifu kuwa, mbali na vifo hivyo, makumi ya watu wengine wamejeruhiwa kutokana na taathira hasi za mafuriko hayo. Maafisa wa serikali ya nchi hiyo wamesema yumkini idadi ya vifo kutokana na janga hilo la kimaumbile ikaongezeka.

Nyumba zaidi ya 25, 961 zimesombwa na mafuriko hayo na kuacha makumi ya maelfu ya watu bila makazi. Kadhalika mafuriko hayo yamesomba mashamba ya kilimo na kuharibu mavuno ya mpunga, jambo ambalo limeliweka taifa hilo la Afrika Magharibi katika hatari ya kukabiliwa na mgogoro wa chakula.

Zaidi ya watu 100 wameaga dunia kutokana na mafuriko nchini Sudan. Aidha zaidi ya 50 nchini Niger

Nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Niger, Sudan, Burkina Faso na Senegal zinashuhudia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha tangu mwezi uliopita wa Agosti.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), hadi sasa watu zaidi ya 103 wameaga dunia katika mafuriko ya Sudan na wengine 56 wamejeruhiwa. Aidha makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na mafuriko hayo katika nchi za  Niger, Burkina Faso na Senegal.