Kenya yasambaratisha mtandao uliotaka kufanya mashambulizi ya biolojia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6355-kenya_yasambaratisha_mtandao_uliotaka_kufanya_mashambulizi_ya_biolojia
Jeshi la polisi la Kenya limesema kuwa, limefanikiwa kusambaratisha mtandao wa madaktari wenye mfungamano na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) uliokuwa na nia ya kufanya mashambulizi makubwa ya silaha za biolojia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 04, 2016 03:23 UTC
  • Kenya yasambaratisha mtandao uliotaka kufanya mashambulizi ya biolojia

Jeshi la polisi la Kenya limesema kuwa, limefanikiwa kusambaratisha mtandao wa madaktari wenye mfungamano na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) uliokuwa na nia ya kufanya mashambulizi makubwa ya silaha za biolojia nchini humo.

Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kenya, Joseph Boinnet alitangaza habari hiyo jana Jumanne.

"Watuhumiwa walikuwa wanapanga kufanya mashambulio makubwa kama yale waliyofanya katika jengo la biashara la Westgate kwa nia ya kuua Wakenya wasio na hatia," amesema, akikusudia shambulio lililofanyika mwezi Septemba 2013 katika jengo hilo la biashara la jijini Nairobi.

Mwezi Septemba 2013, watu wenye silaha walilivamia jengo hilo na kuwashikilia watu kwa muda wa siku nne, tukio ambalo lilipelekea watu 60 kuuawa. Kundi la kigaidi la ash Shabab la nchini Somalia lilitangaza kuhusika na uvamizi huo.

Boinnet amesema, kiongozi wa mtandao huo anajulikana kwa jina la Mohammed Abdi Ali, daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Wote katika Kaunti ya Makueni, kusini mwa Kenya. Alitiwa mbaroni siku ya Ijumaa na anaendelea kushikiliwa na maafisa usalama kwa ajili ya usaili.

Aidha amesema, mtandao huo unaojumuisha wataalamu mbalimbali wa tiba ulikuwa umepanga kufanya mashambulizi nchini Kenya kwa kutumia mada za kemikali za anthrax. Ameongeza kuwa, mtandao huo ulikuwa unakusanya pia wanafunzi wa vyuo vikuu ili wajinge na kundi la Daesh katika nchi za Libya na Syria.