AU yataka Afrika iwe na 'sauti' katika Baraza la Usalama la UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63593-au_yataka_afrika_iwe_na_'sauti'_katika_baraza_la_usalama_la_un
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye ni Mwenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Afrika (AU) amesema muundo wa hivi sasa wa Baraza la Usalama la umoja huo unapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa namna ulivyo hauakisi taswira halisi ya dunia ya leo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 23, 2020 04:48 UTC
  • AU yataka Afrika iwe na 'sauti' katika Baraza la Usalama la UN

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye ni Mwenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Afrika (AU) amesema muundo wa hivi sasa wa Baraza la Usalama la umoja huo unapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa namna ulivyo hauakisi taswira halisi ya dunia ya leo.

Kadhalika Ramaphosa ametoa mwito wa kuongezwa idadi ya nchi za Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Ramaphosa ametoa wito huo alipohutubia mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video hapo jana na kuongeza kuwa, mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja huo yatasaidia katika kusuluhisha migogoro duniani.

Amesema "Umoja wa Mataifa unapoadhimisha miaka 75 tangu kuasisiwa kwake, tunakariri mwito wetu wa kutaka wigo mpana wa uwakilishi kutoka nchi za Afrika katika Baraza la Usalama, na hoja hii izingatiwe kidharura katika mashauriano baina ya serikali.”

Baraza la Usalama la UN

Ramaphosa ameeleza bayana kuwa, ushirikiano baina ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika umesaidia kurejesha amani na usalama katika maeneo ya Darfur nchini Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwenyekiti huyo wa AU amesisitiza kuwa ni kwa kupitia Baraza la Usalama jumuishi na lililofanyiwa marekebisho ndipo kwa pamoja nchi wanachama zitaweza kutatua migogoro iliyodumu kwa miaka mingi duniani.