Uganda ina hamu ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, sayansi na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63609-uganda_ina_hamu_ya_kuimarisha_uhusiano_wa_kiuchumi_sayansi_na_iran
Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga amepongeza uhusiano wa kidugu uliopo baina ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, kuna umuhimu wa kuimarishwa zaidi uhusiano huo katika nyuga za uchumi, sayansi na teknolojia baina ya Kampala ya Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 24, 2020 03:42 UTC
  • Uganda ina hamu ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, sayansi na Iran

Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga amepongeza uhusiano wa kidugu uliopo baina ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, kuna umuhimu wa kuimarishwa zaidi uhusiano huo katika nyuga za uchumi, sayansi na teknolojia baina ya Kampala ya Tehran.

Kadaga amesema hayo katika mazungumzo yake mjini Kampala na Morteza Mortazavi, Balozi wa Iran nchini Uganda. Ameashiria kuhusu uhusiano mzuri wa kibunge ulioko baina ya Uganda na Iran na katika nyuga na taasisi za kimataifa kama vile Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kubainisha kuwa, ushirikiano huo umejengeka katika misingi ya maslahi ya muda mrefu ya pande mbili.

Spika Kadaga wa Bunge la Uganda ameashiria kuhusu safari yake ya kuzitembelea Vyuo Vikuu vya Iran na kueeleza bayana kuwa, fursa za namna hiyo zinapaswa kutumiwa vizuri zaidi. Aidha ametoa mwito wa kupasishwa sheria ya kuboresha ushirikiano wa Tehran na Kampala huku akihimiza juu ya uwekezaji katika nchi mbili hizi rafiki, na vile vile kuondolewa utozwaji wa ushuru mara mbili.

Kwa upande wake, Morteza Mortazavi, Balozi wa Iran jijini Kampala sambamba na kumpongeza Spika wa Bunge la Uganda kwa jitihada zake za kuimarisha uhusiano wa nchi yake na Iran amebainisha kuwa, muswada wa sheria ya kuunga mkono uwekezaji baina ya pande mbili katika nyuga tofauti umeandaliwa. 

Waziri Zarif akipeana mkono na Museveni alipoitembelea Uganda miaka kdhaa nyuma

Aprili mwaka huu, Rais Hassan Rouhani katika mazungumzo yake ya simu na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda aliutaja uhusiano wa Iran na Uganda kuwa mzuri na uliojengeka katika misingi ya heshima, na kusisitiza kuwa Iran iko tayari kuboresha uhusiano wa pande mbili na nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika nyuga zote.

Kwa upande wake, Rais Museveni alisema uhusiano wa Iran na Uganda ni wa kidugu na kirafiki na kubainisha kuwa, kuna umuhimu wa kuimarisha zaidi uhusiano huo wa pande mbili katika nyuga zote.