Mamia ya raia wakamatwa Misri katika maandamano dhidi ya Rais al Sisi
Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Misri yametangaza kuwa mamia ya watu wametiwa nguvuni katika maandamano yanayofanywa na wananchi kwa siku kadhaa mtawalia wakimtaka Rais Abdel Fattah al Sisi ajiuzulu na kuondoka madarakani.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa zaidi ya watu 382 wametiwa nguvuni tangu wananchi wa Misri walipoanza maandamano dhidi ya utawala wa al Sisi tarehe 20 mwezi huu wa Septemba.
Wananchi wa Misri wamekuwa wakifanya maandamano kwa siku ya 9 mfululizo wakitaka kukomeshwa utawala wa kijeshi na kuondoka madarakana Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo.
Maandamano hayo yanafanyika kutokana na wito wa msanii na mfanyabiashara maarufu wa Misri, Muhammad Ali sambamba na hali mbaya ya maisha na kuendelea operesheni ya kubomoa nyumba za raia ambazo serikali ya al Sisi inadai zimejengwa kinyume cha sheria.
Makundi na jumuiya mbalimbali za kisiasa zimeapa kwamba zitaendeleza maandamano hayo hadi Misri 'itakapokombolewa' kutoka kwenye mikono ya maghasibu wa utawala ambao wamesema wamelisaliti taifa, kulidhalilisha jeshi na kuitumbukia nchi katika mikataba ya kifisadi.
Mashirika na jumuiya za kimataifa zinakosoa sana utawala wa al Sisi kutokana na ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu, uhuru wa kisiasa na kijamii na mbinyo mkubwa unaoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.