Wanachama 6 wa Ikhwan wahukukmiwa kunyongwa nchini Misri
(last modified Thu, 01 Oct 2020 02:28:48 GMT )
Oct 01, 2020 02:28 UTC
  • Wanachama 6 wa Ikhwan wahukukmiwa kunyongwa nchini Misri

Mahakama nchini Misri imewahukumu kifo wanachama 6 wa Ikhwanul Muslimin kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya maafisa wa polisi.

Mtandao wa habari wa "al Khaleej al Jadid" umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Jaji wa Mahakama ya Kesi za Jinai ya Zagazig mjini Cairo, Misri jana Jumatano alitoa hukumu ya kifo kwa wanachama 6 wa Ikhwanul Muslimin na kuwafunga miaka kumi kumi wanachama wengine 6 wa kundi hilo.

Mahakama hiyo imedai kuwa watu hao ni wanachama wa kundi lililopiga marufuku, kuwashambulia maafisa wa polisi, kufanya njama dhidi ya serikali, kuwafyatulia risasi polisi na kushiriki katika mauaji ya maafisa wawili wa polisi pamoja na kuiba silaha za moto.

Wanachama wa Ikhwanul Muslimin wakiwa mahakamani Misri

 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hukumu hiyo bado si ya mwisho na inasubiri kuidhinishwa na Mahakama Kuu ya Misri.

Kwa miaka kadhaa sasa mahakama za Misri zimekuwa zikitoa hukumu nyingi za vifo hasa dhidi ya wanachama wa Ikhwanul Muslimin. Taasisi za kisheria zinasema kuwa, sehemu kubwa ya hukumu zinazotolewa dhidi ya wapinzani wa serikali ya Rais Abdel Fattah el Sisi hazitegemei ushahidi wa kweli, bali zinatolewa kwa malengo ya kisiasa.

Mwaka 2013 viongozi wa Misri waliliingiza kundi la Ikhwanul Muslimin katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.

Ukandamizaji mkubwa wanaofanyiwa viongozi na wanachama wa Ikhwanul Muslimin huko Misri umeongezeka baada ya jeshi kumpindua Mohammad Morsi, rais wa kwanza kabisa kuchaguliwa kidemokrasia na wananchi huko Misri. 

Tags