Baraza la Fiqhi la Sudan laharamisha kuanzisha uhusiano na Israel
Baraza la Fiqhi ya Kiislamu la Sudan limesema kuwa haijuzu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Russia Today, wanachama wa baraza hilo la wanazuoni wa Kiislamu nchini Sudan jana Jumatano walipasisha kwa wingi wa kura fatwa inayoharamisha suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel katika uga wowote ule.
Taarifa ya Baraza la Fiqhi ya Kiislamu la Sudan imetolewa katika hali ambayo, Ijumaa iliyopita ya Septemba 25, wananchi wa Sudan walifanya maandamano katika mji mkuu Khartoum kulaani njama za chini kwa chini za kutaka kuanzisha uhusiano na Tel Aviv.
Haya yanajiri huku Marekani ikiendelea kufanya jitihada kubwa za kuzishawishi nchi za Kiarabu na Kiislamu, ikiwemo Sudan, kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.
Mwezi uliopita, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo alifanya safari mjini Khartoum kuwashawishi viongozi wa nchi hiyo wakubali mpango wa kuanzisha uhusino na Israel, lakini inaonekana mazungumzo ya pande hizo mbili hayakuzaa matunda.
Upinzani dhidi ya kuanzisha uhusiano na utawala pandikizi wa Israel ulishtadi nchini Sudan baada ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Baraza la Mpito la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kwenda Imarati mnamo Septemba 20, kujadili na maafisa wa Abu Dhabi kadhia ya kuanzisha uhusiano na Tel Aviv.