Kamanda wa jeshi la Ethiopia: Tunaweza kuzima shambulio dhidi ya al Nahdha
Kamanda wa Jeshi la Anga la Ethiopia amekariri tena kwamba nchi yake ina uwezo wa kuziuia shambulizi lolote dhidi ya bwawa na Renaissance (al-Nahdha) linalojengwa juu ya maji ya Mto Nile ambalo limesababisha mgogoro mkubwa baina ya nchi hiyo na nchi za Misri na Sudan.
Meja Jenerali Yilma Merdasa ameliambia shirika rasmi la habari la Ethiopia kwamba, Jeshi la Anga la nchi hiyo lina uwezo mkubwa na silaha za kisasa na kwamba linakagua kwa makini eneo lote la karibu na bwawa la Renaissance.
Mwezi Machi mwaka huu pia Meja Jenerali Yilma Merdasa alisema kuwa, Ethiopia imejiandaa kukabiliana na shambulizi la aina yoyote. Matamshi hayo yalitolewa baada ya Misri kutishia kwamba itachukua hatua ya upande mmoja iwapo hakutafikiwa mapatano juu ya ujenzi wa bwawa hilo. Wakati huo Ethiopia ilisisitiza kuwa hakuna nchi inayoweza kuizuia kutumia rasilimali zake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kuwa, nchi yake imeazimia kukamilisha mradi wa huo wa ujenzi ulioanzishwa na viongozi wa kabla yake. Amesisitiza kuwa hakuna nguvu yoyote ile inayoweza kusimamisha ujenzi wa bwawa hilo kwa kutumia nguvu. Ameongeza kuwa: "Kama baadhi ya nchi zitatumia makombora, wengine wanaweza kutumia mabomu lakini suala hilo halina maslahi kwetu."
Ujenzi wa Bwawa la Renaissance (al-Nahdha) unaofanywa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile tangu mwaka 2011 umezusha mvutano mkubwa baina ya nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia.
Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini hayajakuwa na matokeo ya kuridhisha.