Amnesty yaitaka serikali ya Misri kusitisha ukandamizaji wa wapinzani
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Misri kukomesha ukandamizaji dhidi ya wapinzani.
Mkuruugenzi wa Kkitengo cha Utafiti na Masuala ya Kisheria kwa Ajili la Magharibi mwa Asia cha Amnesty International, Philip Luther ametoa taarifa akiitaka serikali ya Cairo kuwaachia huru mara moja na bila ya masharti mamia ya watu wanaoshikiliwa korokoroni kwa kosa la kutumia uhuru wao wa kujieleza na kufanya mikusanyiko ya amani.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya kutiwa nguvuni mamia ya wapinzani na kuua baadhi yao katika maandamano ya kupinga utawala wa Rais Abdel Fattah al Sisi yanayofanyika kwa siku kadhaa mtawalia.
Philip Luther amesema kuwa, waandamanaji hao wamejitokeza mitaani na kueleza matatizo yao ya kiuchumi na kijamii licha ya kutambua hatari kubwa ya kupoteza maisha au usalama wao.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa mamia ya Wamisri wametiwa mguvuni tangu wananchi walipoanza maandamano ya kupinga utawala wa rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah al Sisi tarehe 20 mwezi uliopita wa Septemba. Watu wengine kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi na askari usalama.
Tangu aliposhika madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 2013, Abdel Fattah al Sisi amekuwa akikandamiza harakati zote za wapinzani wa serikali akiungwa mkono au kunyamaziwa kimya na nchi za Magharibi hususan Marekani.