Polisi ya Uganda yasema imemkamata Bobi Wine kwa kuvaa magwanda ya kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64026-polisi_ya_uganda_yasema_imemkamata_bobi_wine_kwa_kuvaa_magwanda_ya_kijeshi
Vyombo vya usalama nchini Uganda vimesema lengo la kuvamia makao makuu ya chama cha upinzani cha NUP na kumtia mbaroni Bobi Wine, kinara wa chama hicho anayetazamiwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ni kukusanya magwanda ya kijeshi yanayovaliwa na wafuasi wa chama hicho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2020 04:00 UTC
  • Polisi ya Uganda yasema imemkamata Bobi Wine kwa kuvaa magwanda ya kijeshi

Vyombo vya usalama nchini Uganda vimesema lengo la kuvamia makao makuu ya chama cha upinzani cha NUP na kumtia mbaroni Bobi Wine, kinara wa chama hicho anayetazamiwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ni kukusanya magwanda ya kijeshi yanayovaliwa na wafuasi wa chama hicho.

Msemaji wa Polisi ya Uganda, Fred Enanga amesema mbali na kuvamia makao makuu ya chama hicho, maafisa usalama pia walifanya msako mkali dhidi ya maduka yanayozalisha fulana, buti na kofia zenye nembo za kijeshi za chama hicho katika mitaa ya Kamwokya, Makindye, Kiyembe (Barabara ya Luwum), Mulago, Bwaise na Kawempe jijini Kampala.

Enaga amesema ni kinyume cha sheria za nchi hiyo kwa raia kuvalia mavazi hayo yanayoshabihiana na magwanda ya askari polisi na askari jeshi.

Sajari na kuthibitisha kukamatwa kwa mteja wake, wakili wa Bobi Wine, Anthony Wameli amesema ni jambo la kusikitisha kuona uvamizi wa namna hii unaokiuka misingi ya demokrasia unafanyika mchana peupe na timu kubwa ya maafisa usalama. Amesema lengo la uvamizi huo ni kujaribu kunyamazisha sauti ya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Bobi Wine akizindua chama chake kipya cha NUP

Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, anapigania kuhitimisha utawala wa miaka 34 wa Rais Yoweri Kaguta Museveni katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mapema mwaka ujao 2021.

Mwanamuzi huyo mashuhuri alijiunga na siasa za Uganda mwaka 2017 baada ya kushinda ubunge kupitia uchaguzi mdogo na hatimaye akatangaza nia yake ya kugombea urais.