Sudan yaendelea kushinikizwa ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel
(last modified Sat, 17 Oct 2020 07:19:10 GMT )
Oct 17, 2020 07:19 UTC
  • Sudan yaendelea kushinikizwa ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel

Sudan inaendelea kushinikizwa ili ianzishe uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Marekani imetangaza bayana kuwa, sharti la Sudan kuondolewa katika orodha ya nchi ambazo zinaunga mkono ugaidi ni nchi hiyo kukubali kuanza kufanya mazungumzo yenye lengo la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Hadi sasa wakuu wa Sudan wamekataa kusalimu amri mbele ya Marekani kuhusu kuanzisha uhusiano rasmi na Israel.

Sudan ni moja ya nchi muhimu za Kiarabu, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imeshuhudia mwamko wa wananchi ambao hatimaye ulipelekea kuangushwa utawala wa miaka 30 wa dikteta Omar al Bashir mwaka uliopita wa 2019. Hivi sasa nchi hii muhimu ya Kiarabu imekodolewa macho na Marekani ambayo inataka ifuate nyayo za baadhi ya nchi za Kiarabu katika kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel

Wakuu wa Marekani wanatumia vibaya hali ya kiuchumi ya Sudan na matatizo yanayotokana na hali hiyo kuishinikiza nchi hiyo na kuweka masharti kabla ya kuipa misaada ya kiuchumi.  Kati ya masharti hiyo ni kuwafahamisha wakuu wa Sudan kuwa watapata msaada tu iwapo watafuata bila kuhoji sera za Marekani katika eneo ambapo kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ni sharti la kwanza.

Sadiq al Mahdi, mwenyekiti wa Chama cha Umma cha Sudan ametoa taarifa na kusema: “Kadhia ya kuilazimisha Sudan kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni ni jambo lisilokubalika.”

Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan 

Kwa muda mrefu sasa, Sudan imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 10 nchini Sudan wanakabiliwa na lishe duni na mfumuko wa bei nchini humo hivi sasa umepindukia asilimia 130. Kuibuka janga la corona kumepelekea hali nchini humo izidi kuwa mbaya. Hali hii imepelekea wakuu wa Sudan waanzishe mkakati wa kutaka nchi yao iondolewe katika orodha ya Marekani ya nchi zinazounga mkono ugaidi ili nchi hiyo iweze kupokea mikopo ya Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) na pia misaada ya nchi zingine ikiwemo Marekani.

Hali ya kisiasa na kiuchumi Sudan ni mbaya sana. Kuongezeka uingiliaji wa madola ajinabi, ushirikiano wa wakuu wa Sudan na Saudi Arabia katika kuendeleza vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen na kuuawa mamia ya askari wa nchi hiyo katika vita hivyo ni mambo ambayo yameibua hitilafu kubwa ndani ya nchi hiyo. Hali kadhalika kushindwa serikali ya mpito ya Sudan kufungamana na malengo yake na pia kutotekeleza marekebisho ya kiuchumi kumezidisha matatizo na hivyo kuwafanya wananchi wakosoe vikali utendaji wa serikali hiyo. Katika wiki za hivi karibuni kumeshuhudiwa maandamano ya kulalmikia hali mbaya ya kimaisha kote Sudan.  Wananchi wenye hasira wameandamana katika mji mkuu Khartoum kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi ambapo wanamtaka waziri mkuu Abdullah Hamdok na mwenyekiti wa baraza la mpito Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan waondoke madarakani. Aidha wananchi wenye hasira wamekuwa wakitaka utawala mzima uondoke madarakani kwa kushindwa kutatua matatizo ya kiuchumi.

Hivi sasa wakuu wa Sudan wanakabiliwa na machaguo magumu. Sudan  inaomba msaada wa Marekani na waitifaki wake ili kuboresha hali ya kiuchumi na kisiasa nchini humo. Sudan inahitaji msaada wa dharura wa dola bilioni 1.2 kwa ajili ya kununua ngano na mafuta ya petroli na pia inahitaji mkopo wa dola bilioni mbili kwa ajili ya uthabiti wa kiuchumi. Marekani imeiwekea Sudan masharti ya kupata misaada hiyo na sharti kuu ni kuanzisha uhusiano na Israel. Wananchi waliowengi  wa Sudan wanapinga  vikali nchi yao kuwa na uhusiano na Israel. Si hayo tu bali pia Wasudan waliowengi wanapinga nchi yao kujisalimisha mbele ya Marekani na wametaka wakuu wa serikali ambao wanajikurubisha au kuonyesha kuwa tegemezi kwa Marekani wajiuzulu.

Maandamano ya kupinga serikali nchini Sudan

Abdulrahim Ali, mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Fiqhi ya Kiislamu ya Sudan anasema asilimi 80 ya Wasudan wanapinga uanzishwaji uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo wale wanaounga mkono uhusiano kama huo ni wachache sana. Aidha ametahadharisha kuwa, kuanzisha uhusiano na Israel kutaitumbukiza Sudan katika duru mpya ya machafuko ambayo yatapelekea nchi hiyo ikumbwe na maafa kama yale yanayoshuhudiwa katika nchi jirani ya Libya.

Serikali ya Marekani inajaribu kutumia hali mbaya ya Sudan kufikia malengo yake haramu. Serikali ya Sudan nayo inajaribu kufanya kila inaloweza kubakia madarakani. Kile kilicho wazi ni kuwa haki za taifa la Palestina ni mstari mwekundu kwa wananchi wa Sudan na waliowengi duniani.

 

Tags