Waziri Mkuu wa Sudan: Tunaunga mkono juhudi za kutekelezwa uadilifu
(last modified Mon, 19 Oct 2020 03:04:14 GMT )
Oct 19, 2020 03:04 UTC
  • Waziri Mkuu wa Sudan: Tunaunga mkono juhudi za kutekelezwa uadilifu

Waziri Mkuu wa Sudan amesema katika mazungumzo yake na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwamba nchi yake inaheshimu juhudi za kutekeleza uadilifu duniani.

Abdallah Hamdok amesema hayo wakati alipoonana na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Bi Fatou Bensouda mjini Khartoum na kuongeza kuwa, Sudan inaruhusu kufanyika uchunguzi wa kina kwa ajili ya kusimamishwa uadilifu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mahakama wa Sudan, Nasruddin Abdul Bari, amesema wakati alipoonana na Bensouda kwamba ana uhakika ziara ya Mwendesha Mashataka huyo wa ICC nchini Sudan itakuwa na mafanikio.

Rais wa zamani wa Sudan, Jenerali Omar al Bashir akiwa kizimbani nchini Sudan

 

Bensouda aliwasili nchini Sudan juzi Jumamosi na anatarajiwa kuweko nchini humo hadi keshokutwa Jumatano tarehe 21 Oktoba kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusu masuala yanayohusiana na jimbo la Darfur. Anafuatilia pia suala la kukabidhiwa kwa mahakama ya ICC, rais wa zamani wa nchi hiyo, Jenerali Omar al Bashir anayekabiliwa na tuhuma za kutenda jinai za kivita.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC anafanya juhudi za kufikia makubaliano na viongozi wa Sudan kuhusu kupandishwa kizimbari al Bashir na viongozi wengine kadhaa wa serikali yake katika mahakama hiyo ya kimataifa yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi.

Kabla ya hapo, Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan lilikuwa limetangaza kwamba nchi hiyo haitomkabidhi al Bashir kwa taasisi yoyote ya kimataifa na kwamba kesi zake zote zitasikilizwa ndani ya Sudan.

Tags