Wafadhili wakutana kukusanya dola bilioni 2.4 kwa ajili ya eneo la Sahel
Wafadhili wa kimataifa wamekutana huko Copenhagen, Denmark kuchangisha fedha kwa ajili ya mataifa matatu yaliyo ukanda wa kati wa Sahel barani Afrika ambayo ni Burkina Faso, Niger na Mali kutokana na janga kubwa la kibinadamu linalokabili wakazi wa nchi hizo.
Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 1.5 katika eneo hilo wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na machafuko, idadi ambayo ni mara 20 zaidi ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.
Aidha mbali na hayo, ukatili wa kijinsia umeongezeka, mamilioni ya watoto hawako shuleni na huduma za msingi za afya na kijamii hazipatikani.
Kwa sasa hali ya ukosefu wa chakula ni mara tatu zaidi ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita huku umaskini na mabadiliko ya tabianchi vikitishia mbinu za kawaida za watu kujipatia kipato na hivyo kufanya watu zaidi ya milioni 13 kuhitaji misaada ya kibinadamu.
Miongoni mwao ni watoto milioni 7 walioathiriwa na mapigano sambamba na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
Akizungumzia mkutano huo wa kuchangia fedha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema kunahitajika msaada wa dola bilioni 2.4 ili kusaidia miezi iliyobakia ya mwaka 2020 na kuwapatia watu hao misaada ya dharura hadi mwaka 2021.
Katibu Mkuu huyo amesema msaada wa muda mrefu utapatikana kupitia maendeleo endelevu, utawala bora na fursa sawa kwa wote, hususan kwa vijana.