Magoha: Kesi mpya za Covid-19 hazitapelekea kufungwa shule Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64193-magoha_kesi_mpya_za_covid_19_hazitapelekea_kufungwa_shule_kenya
Waziri wa Elimu wa Kenya George Magoha amekataa suala la kufungwa shule kwa sababu ya kesi mpya za Covid-19 zilizoripotiwa kati ya wanafunzi na walimu baada ya wanafunzi wa darasa la 4, darasa la 8 na Kidato cha Nne kurejea mashuleni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 23, 2020 12:07 UTC
  • Magoha: Kesi mpya za Covid-19 hazitapelekea kufungwa shule Kenya

Waziri wa Elimu wa Kenya George Magoha amekataa suala la kufungwa shule kwa sababu ya kesi mpya za Covid-19 zilizoripotiwa kati ya wanafunzi na walimu baada ya wanafunzi wa darasa la 4, darasa la 8 na Kidato cha Nne kurejea mashuleni.

Prof Magoha, ambaye Ijumaa ya leo alikwenda Kaunti ya Kakamega kukagua vitengo vya uzalishaji wa madawati yanayosambazwa mashuleni, amesema kesi chache za maambukizo ya virusi vya corona mashuleni zinafuatiliwa kwa karibu.

Amesema anatembelea shule kuhakikisha madawati yanakidhi matakwa na yana ubora mzuri kabla ya malipo kushughulikiwa.

Hata hivyo Waziri wa Elimu wa Kenya amedokeza kwamba wanafunzi ambao bado wako nyumbani wanaweza kuchukua muda mrefu kurudi shuleni, akibainisha kuwa hakuna tarehe iliyoainishwa ya kurudi mashuleni wanafunzi hao.

Prof Magoha ameongeza kuwa maambukizo ya virusi vya corona mashuleni ni kielelezo cha hali ya jamii katika baadhi ya maeneo ya Kenya na kwamba kuondolewa vizuizi kumesababisha ongezeko la maambukizo.

Amesema wizara imechukua hatua kuzuia kuenea kwa virusi vya corona na kwamba hakuna "chochote cha kutia wasiwasi".

Kenya ilifungua tena shule kwa wanafunzi wa darasa la 4, darasa la 8 na Kidato cha Nne mapema mwezi huu baada ya shule zote kufungwa kwa kipindi cha miezi saba kutokana na maambukizi ya COVID-19.

Wanafunzi wamerudi mashuleni katika baadhi ya nchi za Afrika

Nchi nyingine kadhaa za Afrika ikiwemo Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimefungua shule baada ya kufungwa kwa miezi kadhaa.

Wakenya wasiopungua 47,843 wameambukizwa virusi vya corona hadi leo Ijumaa na 884 miongoni mwao wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa COVID-19.