Mwandishi habari wa Sudan atahadharisha kuhusu taathira za mapatano na Israel
(last modified Sun, 01 Nov 2020 03:27:31 GMT )
Nov 01, 2020 03:27 UTC
  • Mwandishi habari wa Sudan atahadharisha kuhusu taathira za mapatano na Israel

Mwandishi habari na mchambuzi wa Sudan ametahadharisha kuwa matokeo ya mapatano ya kuanzisha uhusiano kati ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel kupoteza utajiri wa nchi na kuburuzwa.

Mustafa Abdulsalam jana Jumamosi aliandika makala chini ya anwani isemayo: "Chakula Mkabala wa Mapatano" kwamba: Mapatano hayo ambayo yamelazimishwa na nchi za kibeberu hayatakuwa na natija yoyote ya maana kwa Sudan. Abdulsalam ameongeza kuwa, mkabala wake, utawala ghasibu wa Israel utafanya kila uwezalo kutumia mapatano hayo kwa maslahi yake hasa ikingatiwa kuwa, kwa miaka kadhaa Tel Aviv imekuwa ikikodolea macho ardhi yenye rutuba, maji ya kutosha na nguvu kazi nafuu ya Sudan.  

Mwandishi habari na mchambuzi huyo wa Sudan amesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni umedhamiria kustafidi na utajiri wa Sudan kwa kutumia maeneo mengi ya nchi hiyo kwa ajili ya kilimo na hivyo kujitosheleza kwa ngano na vyakula vinginevyo. 

Israel kutumia ardhi ya Sudan kwa maslahi yake

Sudan wiki iliyopita hatimaye ilisalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani na kukubali kuanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel. Baraza la Fiqhi ya Kiislamu la Sudan limetangaza kuwa ni haramu kuanzisha uhusiano wowote na utawala wa Kizayuni mbali na wananchi wa Sudan kuandamana wakipinga uamuzi wa serikali ya mpito ya nchi hiyo wa kuanzisha uhusiano na Israel.

Tags