Harakati ya mapambano ya wananchi ya kukabiliana na Wazayuni yaundwa nchini Sudan
Vyama vya kisiasa, asasi za kiraia na kijamii na makundi ya vijana na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Sudan wameunda kambi ya pamoja ya mapambano ya wananchi kwa ajili ya kukabiliana na uamuzi wa viongozi wa nchi hiyo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, vyama 28, makundi na asasi mbalimbali za Sudan jana Jumamosi zilitia saini makubaliano ya kuunda kambi ya pamoja ya wananchi ya kupambana na hatua ya viongozi wa nchi hiyo ya kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel. Vyama vikuu vinavyoongoza harakati hiyo ni kile cha "al Mutamar al Shaabi" (المؤتمر الشعبی) kwa kimombo Popular Congress Party, harakati ya "Mabadiliko Sasa," chama cha "Jukwaa la Usalama wa Kiuadilifu," jumuiya ya "Vijana Walio Huru" na Jopo la Maulamaa wa Sudan.
Daf'uLlah Taj al Sir, mwakilishi wa harakati ya wananchi amesema mbele ya waandishi wa habari kwamba, Sudan haitonufaika na chochote kwa hatua yake ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zaidi ya uporaji wa utajiri na maliasili za nchi hiyo utakaofanywa na wavamizi hao wa Quds sambamba na kuporomoka maadili.
Hati iliyotiwa saini na vyama, taasisi na jumuiya hizo inasema kwamba, kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel ni ushindi wa kisaikolojia na kisiasa wa utawala dhalimu wa Israel na ni pigo la kikatili kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Tarehe 23 Oktoba 2020, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan chini ya utawala wa mpito wa nchi hiyo ilitangaza kukubali kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa ni nchi ya tano ya Kiarabu. Mwaka 1979 Misri ilitangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni ikafuatiwa na Jordan mwaka 1994 na Imarati, Bahrain na Sudan mwaka huu wa 2020.