Wanigeria waandamana tena kushinikiza kuachiwa huru Sheikh Zakzaky
Wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wameandamana katika mji mkuu Abuja wakilalamikia kuendelea kushikiliwa kizuizini kiongozi wao pamoja na mkewe.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, waandamanaji hao wamejitokeza katika mitaa na barabara mbalimbali za mji mkuu Abuja huku wakiwa wamebeba mabango, maberamu pamoja na picha za Sheikh Zakzaky, ambapo wametoa wito wa kuachiliwa huru haraka kiongozi wao huyo tena bila masharti yoyote pamoja na mke wake.
Wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wanasisitiza kuwa, licha ya utawala wa Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo kufahamu kikamilifu namna hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky inavyozidi kuwa mbaya siku baada ya siku; lakini haujachukua hatua yoyote ya kutatua hali ya kiafya ya mwanazuoni huyo.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.
Hatua kandamizi na za kikatili za polisi na jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky zingali zinaendelea na hadi sasa idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini wamewekwa kizuizini au wameuawa shahidi.
Asasi na jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimeendelea kutoa wito wa kuachiliwa huru kiongozi huyo wa kidini, kama ilivyoagiza mahakama ya nchi hiyo.