Nov 19, 2020 06:55 UTC
  • Boko Haram yatungua helikopta Nigeria na kuua watu 5

Kundi la kigaidi la Boko Haram limetungua ndege aina ya helikopta huko kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua watu watano.

Mashirika mbalimbali ya habari yameripoti kuwa, wapiganaji wa kundi la Boko Haram wametungua helikopta katika eneo la Bama kwenye jimbo la Borno na kuua raia watano. 

Katika siku za hivi karibuni kundi  la Boko Haram limezidisha mashambulia katika maeneo mbalimbali ya umma hususan huko Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na kusababisha hasara kubwa za mali na nafsi.

Kundi hilo lilianzisha harakati zake za kigaidi mwaka 2009 huko kaskazini mwa Nigeria na hadi sasa limepanua hujuma na mashambulizi hayo katika nchi kama Cameroon, Chad na Niger.

Maelfu ya watu wameuawa katika mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi katika nchi hizo. Serikali ya Nigeria inalaumiwa kwa kuzembea kuliangamiza kundi hilo la kigaidi licha ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo kuahidi kwamba, moja ya majukumu muhimu ya utawala wake ni kulisambaratisha kikamilifu kundi hilo.   

Tags