Serikali ya Misri yatakiwa kuwaachia huru wanaharakati 3 wa haki za binadamu
Idadi kubwa ya wahadhiri wa vyuo vikuu na watetezi wa haki za binadamu kote ulimwenguni wamewataka viongozi wa serikali ya Misri iwaachie huru haraka iwezekanavyo wanachama watatu wa taasisi moja ya kutetea haki za binadamu ya nchini humo.
Wahadhiri hao wa vyuo vikuu na shakhsia wa masuala ya sheria kutoka maeneo mbalimbali duniani wanaokaribia 200 wametoa taarifa ya pamoja na kulaaani tuhuma za ugaidi zilizotekelezwa dhidi ya wanachama hao 3 wa Taasisi ya Kutetea Haki za Binadamu ya Misri kwa jina la Egyptian Initiative for Personal Rights. Wahadhiri hao wa vyuo vikuu na shakhsia wa masuala ya sheria wameeleza pia wasiwasi wao kuhusu ukandamizaji mkubwa ulioshudiwa hivi karibuni dhidi ya makundi ya kiraia nchini humo
Taarifa hiyo ya pamoja imeeleza kuwa, askari usalama wa Misri tarehe 15 mwezi huu wa Novemba walimtia mbaroni Mohammed Bashir Mkurugenzi wa Masuala ya Idara wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Egyptian Initiative for Personal Rights.
Pamoja na kulaaniwa na kukosolewa vikali hatua hiyo ya askari usalama wa Misri, lakini askari hao tarehe 18 mwezi huu pia walimtia mbaroni Karim Ennarah Mkurugenzi wa Kitengo cha Kushughulikia Jinai cha taasisi hiyo ya haki za binadamu na kisha tarehe 19 wakamtia mbaroni Gasser Abdul Razzaq Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo ya haki za binadamu.
Umoja wa Mataifa, Amnesty Interenational, Marekani, Canada, Ujerumani, Ufaransa, Italia na Ireland pia zimetoa taarifa kwa nyakati tofauti na kueleza wasiwasi wao kufuatia kutiwa mbaroni wanachama hao 3 wa taasisi hiyo ya haki za binadamu huko Misri; na kuwataka viongozi wa serikali ya nchi hiyo kuwaachia huru watu hao haraka iwezekanavyo.
Wanachama hao watatu wa taasisi hiyo ya Egyptian Initiative for Personal Rights walitiwa mbaroni baada ya kufanya mazungumzo hivi karibuni huko Cairo na mabalozi wa Ujerumani, Denmark, Uhispania, Italia, Ubelgiji, Ufaransa, Finland, Uholanzi, wawakilishi wa Canada, Sweden na Norway, Naibu Balozi wa Marekani na Mwakilshi wa Kamisheni ya Ulaya; ambapo pande hizo zilichunguza njia mbalimbali za kuunga mkono hali ya haki za binadamu huko Misri na ulimwenguni kwa ujumla.