Nigeria inatumia vifaa vya kijasusi vya Israel dhidi ya wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65094-nigeria_inatumia_vifaa_vya_kijasusi_vya_israel_dhidi_ya_wapinzani
Ripoti mpya imefichua kuwa, Shirika la Kijasisi la Jeshi la Nigeria (DIA) linatumia programu ya kijasusi ya Israel kudukua na kupeleleza simu na jumbe fupi za simu za wapinzani na raia wengine nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 09, 2020 08:28 UTC
  • Nigeria inatumia vifaa vya kijasusi vya Israel dhidi ya wapinzani

Ripoti mpya imefichua kuwa, Shirika la Kijasisi la Jeshi la Nigeria (DIA) linatumia programu ya kijasusi ya Israel kudukua na kupeleleza simu na jumbe fupi za simu za wapinzani na raia wengine nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi moja ya utafiti wa kidijatili ya Chuo Kikuu cha Toronto inayojulikana kama Citizen Lab, shirika la Circles la Israel limekuwa likizisaidia serikali za nchi 25, ikiwemo ya Nigeria kuwafanyia ujasusi wapinzani, wanaharakati, waandishi habari na raia wengine.

Ripoti hiyo imebaini kuwa shirika la Circles ni shirika dada la shirika la NSO Group la Tel Aviv, ambalo nalo linamilikiwa na shirika la Pegasus, ambalo limesaidia majasusi wa kiserikali duniani kudukua simu za watu 1,400 katika mabara manne. Kwa mujibu wa taarifa shirika hilo liliwezesha serikali kujipenyeza kwa siri katika simu za watumizi na kuweza kufuatilia utumizi wa kamera, mikrofoni na taarifa zote binafsi zilizo ndani ya simu za mkononi.

Ripoti hiyo imedokeza kuwa yamkini mashirika mawili ya kijasusi ya Nigeria yametumia vifaa  vya Circles kudukua simu za raia wa nchi hiyo.

Gazeti la Premium Times la Nigeria lilifanya uchunguzi na kubaini kuwa magavana wa majimbo mawili ya Nigeria walitimua mfumo wa kijasusi wa Circles kuwachunguza wapinzani.

Shirika la Israel la kudukua simu la Pegasus limehusishwa na udukuzi wa simu Mexico, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.