Watu kadhaa wauawa na kujeruhiwa katika maandamano ya upinzani Zambia
Kwa akali watu wawili wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya wapinzani wa Zambia, kuonyesha uungaji mkono wao kwa kinara wao, Hakainde Hichilema.
Mamia ya wafuasi hao wa Hichilema walikabiliwa vikali na maafisa usalama kwa risasi hai na mabomu ya kutoa machozi, walipokusanyika jana Jumatano nje ya makao makuu ya polisi katika mji mkuu, Lusaka kumuunga mkono Hichilema ambaye ni kinara wa chama kikuu cha upinzani cha UPND na ambaye pia ni mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Mwishoni mwa mwaka 2018, Mahakama ya Katiba Zambia ilitangaza kuwa Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo anaweza kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu ujao unaotazamiwa kufanyika Agosti mwaka ujao 2021.
Lungu alichanguliwa kuwa rais wa Zambia kwa mara ya kwanza Januari mwaka 2015, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Michael Sata, na kisha kuongoza kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita, kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika Septemba mwaka 2016.
Vyama vya upinzani tayari vimekosoa vikali azma ya Lungu ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2021 kwa muhula wa tatu, kwani kisheria, hafai kuwania urais kwa zaidi ya vipindi viwili.
Itakumbukwa kuwa, Rais Lungu, alimshinda kinara wa chama cha upizani cha UPND, Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa mwaka 2016 uliokuwa na ushindani mkali. Hata hivyo Hichelema alikataa kumtambua Lungu kama rais wa Zambia na kusema kura zake ziliibwa.