UN, AU: Kikosi cha UNAMID kimetimiza majukumu Darfur, Sudan
(last modified Sat, 02 Jan 2021 02:45:50 GMT )
Jan 02, 2021 02:45 UTC
  • UN, AU: Kikosi cha UNAMID kimetimiza majukumu Darfur, Sudan

Viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wametoa shukrani zao za dhati kwa kikosi cha kulinda amani cha UNAMID kwa kumaliza kwa mafanikio oparesheni ya kulinda amani huko Darfur, Magharibi mwa Sudan.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika AU, Moussa Faki Mahamat na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wamesema kwa mujibu wa maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Amani la Umoja na Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa, Disemba 31 2020 ilikuwa siku ya mwisho ya oparesheni za Mpango wa Pamoja Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika  wa kulinda amani Darfur Sudan ujulikanao kama UNAMID.

Mahamat na Guterres wamesema kuanzishwa kwa mpango huo wa aina yake miaka takriban 13 iliyopita ilikuwa ni hatua ya kihistoria ambapo mashirika yote mawili AU na UN, nchi zilizochangia wanajeshi na polisi na wahisani wameshiriki katika juhudi za pamoja za kuwalinda rai ana kusaidia ujenzi wa amani Darfur.

Askari wa UNAMID

Mwenyekiti wa Tume ya Au na Katibu Mkuu kwa pamoja wameishukuru UNAMID kwa kazi kubwa. Aidha wamesisitiza kuhusu ahadi yao ya kuendelea kuisadia serikali na watu wa Sudan katika kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika mchakato wa amani na utekelezaji wa mpango wa kitaifa wah atua katika kuwalinda raia.

Pia wametoa wito kwa wadau wote wa Sudan kuhakikisha usalama na mpangilio wa kuondoka kwa mpango wa UNAMID katika kipindi cha miezi sita ijayo na kuruhusu mpango mpya wa usaidizi utakaochukua nafasi ya UNAMID ujulikanao kama UNITAMS.

 

Tags