Jeshi la Uganda laua wanachama 189 wa al Shabab nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66008-jeshi_la_uganda_laua_wanachama_189_wa_al_shabab_nchini_somalia
Jeshi la Uganda UPDF limetangaza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wameua wanachama 189 wa genge la al Shabab katika shambulizi la kushtukiza na la kasi kubwa nchini Somalia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 23, 2021 04:28 UTC
  • Jeshi la Uganda laua wanachama 189 wa al Shabab nchini  Somalia

Jeshi la Uganda UPDF limetangaza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wameua wanachama 189 wa genge la al Shabab katika shambulizi la kushtukiza na la kasi kubwa nchini Somalia.

Katika taarifa yake ya jana Ijumaa, jeshi la Uganda limetangaza kuwa, askari wa nchi hiyo wanaolinda amani huko Somalia chini ya mwavuli wa kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM wamevamia maficho ya genge hilo la kigaidi katika kijiji cha Sigaale, yapata kilomita 99 magharibi mwa mji mkuu Mogadishu na kuua kundi kubwa la wanamgambo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi wa Uganda wamekamata pia silaha pamoja na makamanda wawili wa genge hilo la kigaidi.

Gari la magaidi wa al Shabab lililoteketezwa katika shambulio la anga la jeshi la Uganda UPDF huko Somalia

 

Taarifa ya jeshi la Uganda UPDF imesema, kiwango kikubwa cha zana za kijeshi na vifaa vinavyotumiwa na genge hilo la kigaidi vimeangamizwa. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, jeshi la UPDF limesambaratisha pia mkutano wa genge la al Shabab na kujeruhi magaidi kadhaa katika eneo la  Doncadaafeedow lililoko umbali wa kilomita 7 kutoka mji wa Janaale.

Wanajeshi wa Uganda wako nchini Somalia kwa zaidi ya miaka 10 sasa chini ya mwavuli wa kikosi cha Umoja wa Afrika maarufu kwa jina la AMISOM. Uganda ilikuwa nchi ya kwanza kabisa ya Afrika kutuma wanajeshi wake huko Somalia.

Katika siku za hivi karibuni magaidi wa al Shabab wameshadidisha machambulizi yao hasa kutokana na askari wa AMISOM kwa kushirikiana na Jeshi la Taifa la Somalia kuzidi kukomboa maeneo yanayoshikiliwa na magaidi hao wakufurishaji.