Uturuki kutuma jeshi Afrika Magharibi baada ya meli yake kutekwa nyara
Maharamia wameshambulia meli ya mizigo ya Uturuki katika pwani ya Afrika Magharibi na kuwateka nyara mabaharia 15 na kuua mmoja huku serikali ya Uturuki ikitangaza kuwa itatuma jeshi kuwanusuru mabaharia hao.
Idara ya Usafiri Baharini nchini Uturuki imesema wakati meli iliposhambuliwa, mabaharia walijificha kwa muda wa masaa sita kabla ya maharamia kufanikiwa kuwapata. Katika mapigano yaliyojiri baharia mmoja wa meli hiyo iliyotajwa kuwa MV Mozart alifariki. Mabaharia wote katika meli hiyo ni raia wa Uturuki isipokuwa aliyeuawa ambaye ni raia wa Jamhuri ya Azerbaijan.
Imedokezwa kuwa baada ya maharamia kuwateka nyara mabaharia 15 siku ya Jumamosi, waliondoka katika meli hiyo na kuiacha katika Ghuba ya Guinea ikiwa na mabaharia watatu. Meli hiyo sasa inaelekea katika Bandari ya Gentil ya Gabon.
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amezungumza mara mbili na baharia anayesimamia meli hiyo hivi sasa na ametoa amri ya hatua za haraka kuchukuliwa kuwanusuru mabahari waliotekwa nyara.
Kwa mujibu wa Idara ya Shirika la Kimataifa la Usafiri Baharini, Ghuba ya Guinea, ambayo iko katika pwani za Nigeria, Guinea, Togo, Benin na Cameroni, kwa sasa ni eneo hatari zaidi baharini kutokana na ongezeko kubwa la uharamia.
Julai 2019, mabahari 10 wa Uturuki walitekwa nyara katika pwani ya Nigeria na kuachiliwa huru baada ya mwezi moja.