Meli za Kivita za Iran zazuia hujuma ya maharamia Bab el-Mandeb
(last modified Sun, 03 Jul 2016 03:29:01 GMT )
Jul 03, 2016 03:29 UTC
  • Meli za Kivita za Iran zazuia hujuma ya maharamia Bab el-Mandeb

Meli za kivita za Iran zimefanikiwa kuzuia shambulio kubwa la maharamia ambao walikuwa wanalenga kuiteka meli ya kibiashara ya Iran katika Lango la Bahari la Bab el Mandeb katika Pembe ya Afrika.

Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa taarifa na kusema, mapema Jumamosi maharamia 115 waliokuwa katika meli ndogo 12 walishambulia meli moja ya kubeba mafuta ya Iran wakikusudia kuiteka nyara. Baada ya kupokea ombi la msaada, meli mbili za kivita za Iran zilizokuwa karibu zilifika katika eneo hilo na kukabiliana na maharambia hao ambao walilazimika kutoroka.

Baada ya masaa matatu maharamia walishambulia tena meli hiyo ya kubeba mafuta ya Iran lakini wakatimuliwa kabisa. Manowari hizo za Jeshi la Wanamaji la Iran, zinazojulikana kama Lavan na Shaheed Naqdi, ziliisindikiza meli hiyo ya mafuta hadi eneo salama.

Msafara wa 41 wa Manowari za Jeshi la Wnamaji la Iran ulielekea katika maji ya kimataifa mwezi uliopita wa Juni kwa lengo la kulinda njia za baharini zinazotumiwa na meli za Iran katika maji ya kimataifa.

Katika miaka ya hivi karibuni, Jeshi la Wanamaji la Iran limeimarisha harakati zake katika maji ya kimataifa kwa lengo la kudumisha usalama na kulinda meli za kibiashara na zinazobeba mafuta. Wanamaji wa Iran wamefanikiwa pakubwa kuzuia hujuma kadhaa za maharimia waliolenga kuteka meli za Iran na za mataifa mengine katika maji ya kimataifa.

Tags