Kushadidi malalamiko ya wananchi nchini Sudan
(last modified Tue, 26 Jan 2021 12:12:47 GMT )
Jan 26, 2021 12:12 UTC
  • Kushadidi malalamiko ya wananchi nchini Sudan

Sambamba na kushadidi matatizo ya kiuchumi nchini Sudan, wananchi wa nchi hiyo wameanza tena kufanya maandamano wakilalamikia hali hiyo.

Katika kipindi cha siku tatu zilizopita, mamia ya wananchi wa Sudan wamejitokeza katika mji mkuu Khartoum na miji mingine ya nchi hiyo na kuandamana wakilalamikia uhaba wa mikate na nishati ya umeme. Waandamanaji hao walikusanyika katika barabara kuu ya upande wa mashariki mwa Khartoum ambapo waliweka vizuizi barabarani na kuchoma moto matairi kama njia ya kubainisha hasira zao kufuatia ongezeko kubwa la ughali wa maisha, uhaba wa chakula na kukatika umeme mara kwa mara.

Kundi la Jumuiya ya Wafanyabiashara ambayo ndio iinayoongoza malalamiko hayo, imeeleza kuwa, sera za utawala wa mpya nchini Sudan zinashabihiana na zile za aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir na kutangaza kuwa, serikali sambamba na kutekeleza uadilifu inapasa kuwaunga mkono wafanyazi na wazalishaji wa ndani wa bidhaa.

Sudan kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi na mizozo ya ndani licha ya kuwa na utajiri na vyanzo vingi vya madini. Hali hii imekuwa ikiongeza na kushadidi kadiri siku zinavyosonga mbele, kiasi kwamba, kuongezeka umasikini na ughali wa maisha kuliwafanya wananchi kujitokeza katika maandamano makubwa ya kupinga sera za kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Omar al-Bashir na hatimaye wakamuondoa madarakani.

Omar Hassan al-Bashir, Rais wa zamani wa Sudan

 

Wananchi wa Sudan walikuwa na matumaini kwamba, kuondoka madarakani al-Bashir kungeboresha mazingira ya kisiasa na hali ya uchumi ya nchi. Lakini kinyume na matarajio yao, mabadilikko hayo ya kisiasa ambayo yamepelekea kuingia madarakani serikali ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok, hayajaweza kuwa tiba mujarabu ya kuboresha hali ya mambo ya nchi hiyo. Filihali, Sudan inakabiliwa na hali mbaya mno ya kiuchumi ambapo, uhaba wa chakula, ukosefu wa ajira, wimbi la umasikini, kuendelea mizozo ya ndani, kuendelea vita katika baadhji ya maeneo, kuenea virusi vya Corona na uhaba wa vifaa na suhula za kitiba, dawa na kadhalika ni mambo ambayo yameifanya Sudan kutumbukia katika mgogoro mkubwa.

Mazingira hayo sambamba na uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan, ni mambo ambayo yameifanya serikali ya Khartoum isahahu malengo ya Wasudan ya kufanyika mageuzi na badala yake kunyoosha mkono wa kuomba msaada kwa Marekani na waitifaki wake wa kieneo. Katika fremu hiyo na licha ya upinzani mkali na malalamiko ya wananchi na vyama vya siasa, serikali ya Waziri Mkuu Hamdok ikishinikizwa na Marekani Oktoba mwaka jana ililazimika kuanza mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Abdallah Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan

 

Hamdok alitia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kigaidi wa Israel katika hali ambayo, akthari ya vyama vya siasa vya Sudan vikiwemo vyama viwili muhimu wa al-Mu'tamar al-Watan na al-Baath vilitangaza kupinga vikali mpango huo.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alikuwa na matumaini kwamba, ubadilishaji huu msimamo wa kidiplomasia wa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuchukua misimamo iliyo dhidi ya muqawama wa taifa la Palestina, ungeandaa mazingira ya kuboreka uchumi wa Sudan.

Hata hivyo, kuanzisha uhusiano na Wazayuni, kivitendo hakujawa na matunda kwa Sudan; na Marekani nayo iliyoishawishi na kuishinikiza Sudan kufanya hivyo, haijaipatia fedha na msaada serikali ya Khartoum. Hivi sasa imepita miezi kadhaa tangu Sudan ilipotangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel-Aviv, ambapo Waziri wa Habari wa Sudan ananukuliwa akikiri waziwazi kwamba, kile ambacho kilikuwa kikielezwa kuhusiana na kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kwamba, siasa hizi zingepelekea kupatikana amani na utulivu kwa pande zinazofanya mazungumzo, zilikuwa ni ndoto za alinacha.

Maandamano ya wananchi wa Sudan ya kupinga nchi yao kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel

 

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, msukumo mkubwa wa wale walioukubali mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel nchini Sudan ulikuwa ni kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Khartoum; hii ni katika hali ambayo, ahadi ya Washington haijatekelezwa kivitendo.

Katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kuongezeka ughali wa maisha, kuibuka uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu sambamba na kuongezeka bei ya nishati na mikate, malalamiko na maandamano ya barabarani kwa mara nyingine tena yameanza kushuhudiwa nchini Sudan.

Serikali ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok hivi sasa inakabiliwa na migogoro lukuki kama ya kushadidi vita katika jimbo la Darfur, mzozo wa Bwawa la al-Nahdha na mvutano wa mipaka na jirani yake Ethiopia huko mashariki mwa nchi. Inaonekana kuwa, kama serikali ya Hamdok na washirika wake watashindwa katika kipindi cha muda mfupi kuanzia sasa kuboresha hali ya uchumi wa nchi hiyo, basi watakabiliwa na malalamiko na maandamano ya wananchi yenye wigo mpana zaidi ambayo yatateteresha kama si kubomoa kabisa nafasi zao za uongozi.

Tags