UNHCR yaitaka Sudan Kusini iimarishe usalama ili wakimbizi warejee nyumbani
(last modified Sat, 30 Jan 2021 04:26:01 GMT )
Jan 30, 2021 04:26 UTC
  • UNHCR yaitaka Sudan Kusini iimarishe usalama ili wakimbizi warejee nyumbani

Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Filippo Grandi ameitaka Sudan Kusini kuimarisha usalama, utawala wa sheria na uongozi bora ili kuweka mazingira mazuri kwa wakimbizi kurejea makwao.

Akizungumza na wanahabari mjini Juba, Grandi amesema mamilioni ya raia wa Sudan Kusini wako uhamishoni nje ya nchi ma wamekuwa wakimbizi wa ndani, lakini idadi kubwa wanarejea makwao, na changamoto zinazowakabili ni umasikini, masuala ya ardhi, na uhaba wa huduma za kijamii.

Kuna zaidi ya wakimbizi milioni mbili kutoka Sudan Kusini wanaoishi katika nchi jirani za Kenya, Sudan, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Grandi amesema hali ya usalama kwa sasa nchini Sudan Kusini ni nzuri kuliko ilivyokuwa mwaka 2017, alipotembelea nchi hiyo kwa mara ya mwisho, hata hivyo amesema, sehemu za nchi hiyo bado hazifikiwi kwa urahisi kutokana na ukosefu wa usalama.  Grandi pia ametoa wito kwa serikali ya mpito ya Sudan Kusini kuharakisha utakelezwaji wa mchakato wa amani wa mwaka 2018.

 

Tags