Waziri Mkuu wa Sudan avunja baraza lake la mawaziri
Waziri Mkuu wa Sudan Abdullah Hamdok amevunja baraza lake la mawaziri. Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Hamdok amesema mawaziri watabakia katika nafasi zao kwa ajili ya kutekeleza majukumu katika wizara zao hadi wakati wa kuundwa serikali mpya na shughuli ya ukabidhianaji wizara kukamilika.
Inatarajiwa kuwa Hamdok atatangaza baraza lake jipya la mawaziri baadaye leo. Wiki iliyopita Sudan ilitangaza kuwa wawakilishi watatu wa makundi ya waasi watapata nafasi katika serikali ya muda kama sehemu ya mapatano ya amani yaliyotiwa siani mwaka jana.
Sudan iko katika kipindi cha mpito cha kuelekea utawala kamili wa kidemokrasia baada ya mwamko ambao ulimuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Omar al Bashir mwaka 2019.
Hayo yanajiri wakati ambao katika siku za hivi karibuni, wananchi wa Sudan wamekuwa wakiandamana katika mji mkuu Khartoum kupinga uamuzi wa watawala wa nchi hiyo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuendelea serikali ya mpito na mchakato wa kuwa na uhusiano wa kawaida na Wazayuni ambao mikono yao imejaa damu za Waarabu na Waislamu wasio na hatia.
Waandamanaji wamechoma moto bendera za utawala huo dhalimu katika mitaa ya Khartoum na kupiga nara za kutangaza upinzani wao kwa hatua ya viongozi wa serikali ya mpito ya kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel.
Aidha wananchi wa Sudan pia waliandamana mara kadhaa mwaka uliopita wakilalamikia ugali wa maisha.
Mwezi uliopita, waandamanaji hao walikusanyika katika barabara kuu ya upande wa mashariki mwa Khartoum ambapo waliweka vizuizi barabarani na kuchoma matairi kama njia ya kubainisha hasira zao kufuatia ongezeko kubwa la ughali wa maisha, uhaba wa chakula na kukatika umeme mara kwa mara.
Hivi sasa pia kutokana na janga la COVID-19, Sudan yenye idadi ya watu milioni 40, inakumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Wananchi wanalazimika kupanga foleni masaa kadhaa kununua mkate huku kukiwa na uhaba mkubwa wa umeme. Ughali wa maisha ulifika asilimi 269 mwezi jana huku nchi hiyo ikiwa na deni la zaidi ya dola bilioni 60.