Waziri Mkuu wa Sudan atangaza baraza jipya la mawaziri
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok ametangaza baraza jipya la mawaziri la serikali yake.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, katika baraza hilo jipya la mawaziri, Maryam Sadiq al-Mahdi, binti wa Sadiq al Mahdi, kiongozi wa chama cha upinzani cha Ummah aliyefariki dunia hivi karibuni, ameteuliwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje wa nchi hiyo.
Hamdok ameeleza pia kuwa, Jibril Ibrahim, kiongozi wa kundi la waasi wa Darfur la Uadilifu na Usawa atakuwa waziri wa fedha katika serikali hiyo mpya.
Mapema wiki hii, Abdalla Hamdok, alitangaza kuvunjwa baraza la mawaziri la serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa na ofisi ya waziri mkuu huyo wa Sudan, mawaziri wote wa serikali ya mpito wameuzuliwa lakini wataendelea kuongoza wizara zao hadi litakapoundwa baraza jipya la mawaziri.
Serikali mpya ya sasa ya mpito ya Sudan itakuwa na wizara 26, ambapo makundi ya wabeba silaha yataongoza wizara saba kati ya hizo.
Uundaji wa serikali mpya ya mpito ya Sudan umefanyika kwa msingi wa utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa miezi michache iliyopita kati ya serikali na makundi yanayobeba silaha.
Tarehe 3 Novemba 2020 baraza la utawala na baraza la mawaziri la Sudan yaliifanyia marekebisho hati ya katiba ya nchi hiyo ambayo yalirefusha muda wa kipindi cha mpito kwa miezi ipatayo 14.../