Kesi ya uchaguzi; Mahakama ya Juu ya Uganda yakataa ombi la Wine
Mahakama ya Juu ya Uganda imetupilia mbali ombi la mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, la kutaka kufanyia marekebisho faili lake la kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyompa ushindi Rais Yoweri Museveni.
Majaji wa mahakama hiyo wakiongozwa na Jaji Mkuu Alfonce Owiny Doro wamekataa kukubali ombi hilo la Wine kwa msingi kuwa limewasilishwa nje ya muda ulioanishwa na sheria za nchi hiyo.
Hapo jana mawakili wa Wine waliitaka Mahakama ya Juu iwaruhusu kuwasilisha ushahidi zaidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita wa Januari.
Mapema jana, Rais Museveni, Tume ya Uchaguzi kupitia mawakili wake na Mwanasheria Mkuu, William Byaruhanga waliiomba mahakama hiyo isilikubali ombi hilo la mawakili wa Wine.
Hata hivyo majaji hao wa mahakama hiyo ambayo ndiyo ya juu zaidi nchini Uganda wamesema wataendelea kuyasikiliza maombi yaliyowasilishwa hapo awali na mawakili wa Wine.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Museveni alishinda uchaguzi huo Januari 16 kwa kura milioni 5.85 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote wakati mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi aliyegombea kupiti chama cha NUP akipata kura milioni 3.48 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.