Kuendelea maandamano dhidi ya serikali kote Sudan
Baada ya kupita miaka miwili tokea uanze mgogoro wa Sudan ambao ulipelekea kuondolewa madarakani Rais Omar Al Bashir mnamo Apirli 2019, nchi hiyo ingali inaendelea kushuhudia migogoro kadhaa ya kisiasa, kichumi na kiusalama.
Hali mbaya nchini humo kwa mara nyingine imepelekea wananchi wajitokeze mitaani kuandamana kulalamikia hali ya mambo. Katika siku za hivi karibuni aghaalbu ya miji mikubwa Sudan imeshuhudia maandamano ya wananchi wenye hasira wanaolamikia utendaji kazi wa serikali ya mpito.
Maandamano ya wananchi Sudan yalianza Disemba 19 2018 kwa kisingizio cha ongezeko la bei ya mkate na mafuta ya petroli. Maandamano hayo yaligeuka na kuwa malalamiko ya kisiasa na hatimaye yakapelekea kuondolewa madarakni mtawala wa muda mrefu Omar al Bashir. Wanajeshi wa nchi hiyo walichukua madaraka lakini maandamano ya wananchi yaliendelea kwa lengo la kutaka raia wakabidhiwe madaraka. Hatimaye Agosti 2019, jeshi lilitangaza kuundwa serikali ya mpito yenye kujumuisha raia ili kutuliza mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini humo katika kipindi cha mpito cha kuelekea uchaguzi. Lakini hivi sasa baada ya kupita takribani mwaka mmoja na nusu tokea iundwe serikali ya mpito Sudan kwa mara nyingine inashuhudia maandamano ya wananchi wenye hasira.
Kwa hakika serikali ya mpito inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdullah Hamdok imeshindwa kupata mafanikio katika uga wa kiuchumi na kisiasa.
Matatizo ya kiuchumi yanaendelea kuikumba Sudan ambayo tayari ilikuwa na mgogoro wa umasikini na ukosefu wa ajira. Hivi sasa nchi hiyo inakumbwa na uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu ambazo hutumiwa na wananchi kila siku mbali na ongezeko kubwa la bei ya mafuta ya petroli na mkate. Wananchi wa Sudan walikuwa na matumaini kuwa mabadiliko ya kisiasa nchini humo yangeweza kuboresha hali ya kiuchumi lakini hakuna chochote kilichoboreka.
Badala ya serikali ya Sudan kujitahidi kuboresha miundomsingi ya kichumi nchini humo imejikita katika kutegemea misaada ya madola ya kigeni. Ni kwa msingi huo ndio kwa kuhadaiwa kuwa itapokea misaada ya kifedha ya Markeani, serikali ya Sudan iliafiki kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kile kilichotajwa kuwa ni 'Mapatano ya Ibrahim'.
Pamoja na kuwa uamuzi kama huo haukutarajiwa kutoka kwa wakuu wa Sudan, si tu kuwa nchi hiyo haijapokea misaada ya kifedha kama ilivyotarajia bali pia uamuzi huo umepelekea kushadidi hitilafu za kisiasa ndani ya Sudan. Hata Feisal Mohammad Salih, Waziri wa Habari wa Sudan amekiri kuwa, serikali ya Marekani ilitangaza kuwa sharti la kuondolewa Sudan katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi ni kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel. Ameongeza kuwa, ni ndoto kudhani kuwa kuanzisha uhusuano wa kawaida na Israel kutaleta amani na utulivu.
Wananchi wa Sudan wamekasirishwa sana na utendaji kazi wa serikali ya mpito kwani walitaraji kuwa kwa kuondolewa utawala wa kidikteta wa al Bashir hali ingeboreka lakini sasa hali inazidi kuwa mbaya. Hivi sasa Wasudan waliowengi wamepoteza matumani kufuatia utendaji mbovu wa serikali ya mpito na kwa hivyo wamemiminika mitaani kubainisha malalamiko hayo. Wasudan wengi wanaamaini kuwa serikali ya mpito imeondoka katika mkondo wa malengo ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani al Bashir.
Serikali ya mpito ya Sudan imefanya mabadiliko katika baraza la mawaziri hivi karibuni kwa lengo la kuwatuliza wananachi wenye hasira. Aidha katika siku za hivi karibuni vinara wengi wa chama kilichovunjwa cha Kongresi ya Kitaifa ambacho kilikuwa chama cha al Bashir wamekamatwa. Serikali ya mpito inadai kuwa wanachama hao wa Kongresi ya Kitaifa wamekuwa wakiwachochea wananchi kuandamana na kufanya uharibifu katika maeneo ya biashara na miundo msingi. Hivi sasa hali ya hatari imetangazwa katika mikoa saba ya Sudan.
Serikali ya mpito inajaribu kutuliza hali ya mambo na inajaribu kuondoa lawama dhidi yake lakini ukweli ni kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua za kivitendo kuboresha hali ya kisiasa na kiuchumi nchini humo. Weledi wa mambo wanaamini kuwa serikali ya mpito ya Sudan haina uwezo wa kuboresha hali ya mambo kwa sasa.
Sayyid Qassim Zakeri, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema Sudan inaelekea katika duru mpya ya ukosefu wa usalama, ghasia na machafuko. Kuna uwezekano mkubwa kuwa Sudan itakumbwa na hatima sawa na ya Somalia na Yemen.
Inaelekea kuwa, serikali ya Hamdok ambayo ilielekeza matumaini yake kwa nchi za Magharibi sasa haina muda wa kutosha wa kukidhi matakwa ya wananchi wanamapinduzi wa Sudan.