Umoja wa Afrika waanza upatanishi katika mzozo wa Sudan na Ethiopia
(last modified Thu, 18 Feb 2021 11:00:39 GMT )
Feb 18, 2021 11:00 UTC
  • Umoja wa Afrika waanza upatanishi katika mzozo wa Sudan na Ethiopia

Duru za kuaminika nchini Sudan zimeripoti kuwa, mjumbe wa Umoja wa Afrika alitazamiwa kuwasili Khartoum akiongoza ujumbe wa upatanishi wa umoja huo katika mzozo wa mpakani baina ya Sudan na Ethiopia.

Mohamed El Hassan Ould Labat alitazamiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Sudan, Abdullah Hamdok na Mkuu wa Baraza la Utawala nchini humo, Abdel Fattah al-Burhan kwa ajili ya kupunguza mzozo ulioibuka baina ya nchi hizo mbili.

Ziara ya Ould Labad mjini Khartoum inafanyika baada ya Sudan kumwita balozi wake nchini Ethiopia Jumatano ya jana kwa mashauriano, kutokana na kuongezeka mzozo wa mpaka baina ya pande hizo mbili ambao umepelekea kutumwa majeshi ya nchi mbili karibu na maeneo ya mpakani katika wiki za hivi karibuni.

Jumapili iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilisema kwamba vikosi vya jeshi la Ethiopia vimevuka mpaka na kuingia Sudan, ikionya kuhusu "athari mbaya" za suala hjilo kwa usalama na utulivu wa eneo hilo.

Mzozo wa mpaka kati ya nchi hizo mbili umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni baada ya Sudan kupeleka vikosi vya jeshi kwenye ardhi ambayo ilisema ilikaliwa kwa mabavu na wakulima wa Ethiopia na wanamgambo wa nchi hiyo.

Majeshi ya Sudan katika mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia

Sudan inadai kuwa, tangu mwezi Desemba mwaka uliopita, zaidi ya Wasudani 12, pamoja na wanajeshi, wameuawa katika mashambulio ya mpakani ya vikosi vya jeshi la Ethiopia katika Jimbo la Gedaref.

Hivi karibuni serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwa imekubali upatanishi wa nchi nyingine katika mgogoro baina yake na nchi jirani ya Sudan lakini kwa masharti. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Dina Mufti aliitaka serikali ya Sudan ikomeshe mashambulizi na kuwafukuza raia wa Ethiopia katika maeneo yao katika operesheni zilizoanza tarehe 6 Novemba wakati Addis Ababa ilipokuwa ikirejesha utawala wa sheria katika eneo la Tigray.

Nchi mbili za Sudan na Ethiopia zinatuhumiana kushambulia na kukalia kwa mabavu ardhi ya kila mmoja wao, tuhuma ambazo zinatishia mustakabali wa uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.

Tags