Ethiopia yataka kutatuliwa hitilafu za mpaka na Sudan kwa njia za amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67486-ethiopia_yataka_kutatuliwa_hitilafu_za_mpaka_na_sudan_kwa_njia_za_amani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ethiopia amesema kuwa, Addis Ababa inataka kutatua hitilafu zake za mpaka na Sudan kwa njia za amani na haitaingia vitani kutokana na kadhia hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 04, 2021 00:45 UTC
  • Ethiopia yataka kutatuliwa hitilafu za mpaka na Sudan kwa njia za amani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ethiopia amesema kuwa, Addis Ababa inataka kutatua hitilafu zake za mpaka na Sudan kwa njia za amani na haitaingia vitani kutokana na kadhia hiyo.

Dina Mufti ameyasema hayo kutokana na kushadidi hitilafu za mpaka kati ya Ethiopa na nchi jirani ya Sudan na kuongeza kuwa: Ni jambo lililombali kutokea vita baina ya pande hizi mbili katika mzozo huu wa mpaka. 

Kuhusu faili la ujenzi wa bwawa na Renaissance juu ya maji ya Mto Nile, Dina Mufti amesema kuwa, Addis Ababa inaendelea kuheshimu na kushikamana na usimamizi wa Umoja wa Afrika wa mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mzozo huo. 

Dina Mufti

Bwawa la al-Nahdha linajengwa katika umbali wa kilomita 15 kutoka kwenye mpaka wa Ethiopia na Sudan. Serikali ya Ethiopia inasema kuwa, karibu asilimia 80 ya ujenzi wa bwawa hilo umekamilika. Litakapoanza kufanya kazi, bawa hilo litakuwa kituo kikuu zaidi cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji duniani.

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini hayajakuwa na matokeo ya kuridhisha pande zote.