HRW: Wanajeshi wa Eritrea wameua mamia ya watoto Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67594-hrw_wanajeshi_wa_eritrea_wameua_mamia_ya_watoto_ethiopia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema wanajeshi wa Eritrea wameua mamia ya raia wakiwemo watoto wadogo katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 06, 2021 23:37 UTC
  • HRW: Wanajeshi wa Eritrea wameua mamia ya watoto Ethiopia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema wanajeshi wa Eritrea wameua mamia ya raia wakiwemo watoto wadogo katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Ripoti ya HRW imesema kuwa, wanajeshi wa Eritrea kwa mpangilio maalumu waliwashambulia wakazi wa mji wa Axum katika eneo la Tigray mwezi Novemba mwaka uliopita 2020, na kuua mamia miongoni mwao wakiwemo watoto wadogo.

Ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu imeongeza kuwa, baada ya kuingia katika mji wa Axum mnamo Novemba 20 mwaka jana, wanajeshi wa Eritrea walianza kutekeleza ukatili huo wa kutisha, na mara nyingi askari wa Ethiopia walitazama tu unyama huo ukiendelea.

Maelezo yaliyoko katika ripoti ya Human Rights Watch yanashabihiana na ya ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Amnesty International juu ya jinai zilizofanywa Novemba mwaka jana na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea katika eneo la Tigray linaloshuhudia mapigano kwa zaidi ya miezi minne sasa.

Mapigano katika eneo la Tigray linalohusisha askari wa Ethiopia, Eritrea na harakati ya TPLF

Licha ya kuendelea kushuhudiwa umwagaji damu katika eneo la Tigray kwa miezi kadhaa sasa, lakini hadi sasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijalaani wala kutoa taarifa ya kutaka kusitishwa mapigano na mauaji hayo.

Alkhamisi iliyopita, Michelle Bachelet, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema ofisi yake ina ithibati ya kufanyika jinai za kutisha ambazo zinaweza kuwa jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea katika eneo la Tigray. Mbali na maelfu ya watu kuuawa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao huko kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo ya eneo la Tigray.