Ufaransa na Ivory Coast zasisitiza kuimarishwa ushirikiano
Ufaransa na Ivory Coast zimesisitiza udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili. Rais François Hollande wa Ufaransa na mwezake wa Ivoy Coast, Alassane Ouattara ambao wamekutana mjini Paris wameeleza pia wasiwasi wao kuhusu harakati za kigaidi hususan katika eneo la magharibi mwa Afrika.
Viongozi hao wawili pia wametoa wito wa kuzidishwa ushirikiano katika masuala ya usalama kwa shabaha ya kuzuia mashambulizi ya kigaidi. Vilevile wametaka kuzidishwa ushirikiano wa kiuchumi wa Paris na Abidjan.
Katika mazungumzo ya marais hao wawili, François Hollande ameashiria kesi inayoshughulikia jinai zilizofanywa na rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo na ametoa wito wa kufuatiliwa kwa makini faili hilo na kushughulikiwa wale wote waliohusika na machafuko ya mwaka 2010 nchini Ivory Coast ambayo yalisababisha mauaji ya watu wasiopungua elfu tatu.
Wachambuzi wa mambo wanasema, Alassane Ouattara ambaye Oktoba mwaka jana alianza kipindi cha pili cha uongozi wake nchini Ivory Coast, anafanya jitihada za kuboresha zaidi uchumi na hali ya usalama nchini humo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, katika kampeni zake za uchaguzi, Ouattara aliahidi kuboresha uchumi. Ivory Coast pia inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo hususan yale ya mpakani.
Wachambuzi wanasema baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka jana, Alassane Ouattara anafanya bidii za kuimarisha uhusiano wa nchi yake na nchi za Ulaya hususan Ufaransa. Katika upande mwingine Paris daima imekuwa ikifanya jitihada za kuzidisha ushawishi wake barani Afrika na inatumia fursa na uwezo wake wote kufanikisha lengo hilo. Baadhi ya wapinzani wa Rais Ouattara pia wanasema alifanikiwa kushinda uchaguzi uliopita kutokana na msaada mkubwa wa Ufaransa, suala linalokadhibishwa na kambi ya kiongozi huyo.
Weledi wa mambo wanasema, licha ya kupita zaidi ya miaka 50 sasa tangu nchi nyingi za Kiafrika zijikomboe kutoka kwenye makucha ya Ufaransa lakini Paris bado ina ushawishi mkubwa katika siasa za nchi zinazozungumza Kifaransa barani humo. Ukweli huo unatiwa nguvu zaidi na uingiliaji wa Ufaransa katika migogoro mingi ya kisiasa katika nchi za Afrika.
Kwa sasa ambapo Paris inakabiliwa na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira na matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, Ufaransa inakodolea macho zaidi utajiri na maliasili za Afrika kuliko wakati wowote mwingine. Ivory Coast ni mzalishaji mkubwa zaidi wa kakao duniani na ina utajiri wa madili kama dhahabu na almasi, mafuta na mazao ya kilimo. Haya yote yameitia Ufaransa hamu kubwa zaidi na kujielekeza nchini Ivory Coast na kuzidisha ushawishi wake nchini humo.
Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, kuwepo zaidi Ufaransa nchini Ivory Coast na ushawishi mkubwa zaidi wa Paris nchini humo unaozidishwa chini ya mwavuli wa kuimarisha amani na kupambana na ugaidi vinaweza kuwa nikabu na pazia la kuficha malengo halisi ya kikoloni ya serikali ya Paris nchini humo na katika nchi nyingine za bara la Afrika.