Rais anayeondoka wa Niger ashinda Tuzo ya Mo Ibrahim
Rais anayeondoka wa Niger, Mahamadou Issoufou ndiye mshindi wa tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim.
Katika taarifa, Wakfu wa Mo Ibrahim umesema, Issoufou ameonyesha uongozi wa ina yake na wa hali ya juu sambamba na kuheshimu demokrasia licha ya changamoto tele.
Festus Mogae, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Mo Ibrahim na rais wa zamani wa Botswana amesema, licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kiuchumi, na hata mashambulizi ya makundi ya kufurutu ada, Rais Mahamadou Issoufou ameliongoza taifa lake katika njia ya ustawi.
Baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo, Issoufou ambaye amehudumu kwa mihula miwili ya urais ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, tuzo hiyo inatoa motisha ya kuendelea kuheshimiwa thamani za demokrasia na uongozi mzuri, si tu Niger na barani Afrika, bali kote duniani kwa ujumla.
Tuzo hiyo ambayo tangu kuasisiwa kwake mwaka 2006 imetunukiwa viongozi sita pekee, huwalenga marais ambao walichaguliwa kwa misingi ya demokrasia na kuhudumu katika muhula ulioanishwa na katiba pasina kung'ang'ania madaraka wala kuongoza kwa mkono wa chuma.
Rais mstaafu wa mwisho kutuzwa tuzo ya Mo Ibrahim ni rais wa zamani wa Liberia Bi Ellen Johnson Sirleaf aliyewahi kushinda pia tunzo ya amani ya Nobel na ambaye pia ni mwanamke wa kwanza Mwafrika kuwahi kuchaguliwa kuwa rais wa nchi. Wengine ni Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014), Pedro Pires wa Cape Verde (2011), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Joaquim Chissano wa Msumbiji (2007).
Mshindi wa tuzo hii hukabidhiwa dola milioni 5 pesa taslimu katika muda wa muongo mmoja hivi na kisha dola laki mbili kila mwaka katika kipindi cha uhai wake.