Kususiwa kikao cha Bunge la DRC na Wabunge wa Kivu Kaskazini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6802-kususiwa_kikao_cha_bunge_la_drc_na_wabunge_wa_kivu_kaskazini
Wabunge wa jimbo la Kivu kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesusia kikao cha Bunge wakilalamikia ukosefu wa amani unaoshuhudiwa katika jimbo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2016 06:34 UTC
  • Kususiwa kikao cha Bunge la DRC na Wabunge wa Kivu Kaskazini

Wabunge wa jimbo la Kivu kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesusia kikao cha Bunge wakilalamikia ukosefu wa amani unaoshuhudiwa katika jimbo hilo.

Mauaji dhidi ya raia katika baadhi ya majimbo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamepelekea wawakilishi wa jimbo la Kivu Kaskazini katika Bunge la nchi hiyo wasusie vikao hatua ambayo imepelekea akthari ya Wabunge kutangaza kufungamana na Wabunge hao.

Wawakilishi wa Kivu Kaskazini katika Bunge la DRC wamechukizwa na upuuzaji unaofanywa na viongozi wa serikali ya Kinshasa kuhusiana na usalama wa majimbo yanayokabiliwa na machafuko.

Wabunge hao wanaamini kuwa, serikali na jeshi hawachukui hatua za lazima za kung'oa mizizi ya makundi yanayobeba silaha ambayo yanaendesha harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wabunge hao wanasisitiza kwamba, kuna haja ya kufanyika operesheni kubwa ya kijeshi kama ilie iliyofanywa dhidi ya waasi wa M23 iliyopelekea kusambaratika waasi hao.

Takwimu za Asasi ya Kiraia ya Congo DR zinaonesha kuwa, kuanzia mwaka 2014 takribani watu 1017 wameuawa na makundi ya waasi katika maeneo ya Beni na Lubero yaliyoko katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Mauaji dhidi ya raia mashariki mwa Jamhuri mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aghlabu hufanywa na waasi wa Uganda na Rwanda wanaoendesha harakati zao katika maeneo hayo.

Hivi karibuni waasi wa Uganda walifanya mashambulio dhidi ya kituo cha jeshi kaskazini mwa Goma makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini; hata hivyo walilazimika kurejea nyuma kutokana na kukabiliwa na upinzani mkali wa wanajeshi wa serikali. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wasimamia amani wa kimataifa walioko mashariki mwa Congo DR wakashadidisha operesheni za kijeshi dhidi ya waasi hao.

Vurugu na machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamesababishwa kusitishwa shughuli za Shirika la Msalaba Mwekundu katika mji wa Rutshuru ulioko katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Wakazi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wamekuwa wakishuhudia mauaji dhidi ya raia yanayofanywa na wanamgambo wa Ituri, juma lililopita waliwataka viongozi wa serikali wadhamini usalama wa raia katika eneo hilo.

Katika mazungumzo yao na ujumbe wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO, walitoa wito wa kurejeshwa amani katika maeneo hayo. Ujumbe huo wa MONUSCO ulikuwa umefanya safari mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa shabaha ya kutathmini hali ya usalama katika maeneo hayo.

Wajumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nao wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Filihali, hatua ya Wabunge wa jimbo la Kivu Kaskazini ya kususia vikao vya Bunge ni malalamiko ya wazi ya wawakilishi hao wa wananchi kwa serikali. Lililobaki sasa ni kuona nini itakuwa radiamali ya serikali kwa hatua ya wawakilishi hao wa Bunge.